LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali iko tayari kuboresha maslahi ya mabaharia

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Suleiman Makame amesema Serikali iko tayari kuboresha zaidi maslahi ya mabaharia pamoja na mazingira yao ya kazi.

Waziri Makame ameyasema hayo Alhamisi Juni 22, 2023 wakati akifungua maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza akimwakilisha Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman.

“Serikali iko tayari kufanyia kazi ombi lenu kuhusu maslahi duni kwa mabaharia, anzeni kutoa maoni nasi Serikali tutayafanyia kazi” amesema Waziri Makame huku akiwahimiza waajiri kuweka mazingira rafiki ya kazi kwa mabaharia hususani wanawake wakati wa kujistiri.

Katika hatua nyingine Waziri Makame amepongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuboresha miundombinu ya usafiri wa majini ikiwemo ujenzi wa meli mpya ya MV. Mwanza pamoja na ukarabati wa meli ya MV. Mapinduzi II.

Akizungumza kwa niaba ya mabaharia, Katibu Chama cha Mabaharia Zanzibar, Ally Mzee amesema kada hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira za uhakika, maslahi duni, mazingira rafiki kazini hususani kwa wanawake pamoja na vyama kushindwa kuwatetea mabaharia wanapokumbana na changamoto kazini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Amosi Makalla amesema utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maziwa na bahari itachochea ajira kwa kada ya mabaharia akitolea mfano ujenzi wa meli mpya ya MV. Mwanza ambayo imefikia asilimia 84.

Maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani yanafanyika kitaifa katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza kuanzia Juni 22-25, 2023 ambapo yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji elimu usalama majini, kufanya usafi katika fukwe za Ziwa Victoria pamoja na mbio ya riadha itakayowashirikisha mabaharia yakiambatana na kauli mbiu isemayo “Miaka 50 ya Marpol, uwajibikaji unaendelea”.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Suleiman Makame akifungua maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza kuanzia Juni 22-25, 2023. Waziri Makame amemwakilisha Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Amos Makalla (hayuko pichani) kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), King Chiragi akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani 2023 yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Wadau mbalimbali wakifuatilia ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza ambapo kilele ni Jumapili Juni 25, 2023.
Msimamizi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Zanzibar (ZMA), Sheikha Mohamed akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Katibu Chama cha Mabaharia Zanzibar, Ally Mzee akizungumza kwa niaba ya mabaharia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Dunia 2023 yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza kuanzia Juni 22-25, 2023.
Kila mwaka Juni 25 huwa ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani ambapo mwaka huu kitaifa maadhimisho hayo yanafanyika jijini Mwanza.
Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Suleiman Makame (wa kwanza kulia) akisikiliza ufafanuzi wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na mabaharia wakati akitembelea na kukagua mabanda kwenye ufunguzi wa Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Suleiman Makame akikagua na kutembelea mabanda mbalimbali kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani 2023 yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Washiriki mbalimbali wakiwemo mabaharia wakiwa kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Viongozi mbalimbali jukwaa kuu wakifuatilia ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Viongozi mbalimbali jukwaa kuu wakifuatilia ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani 2023 yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Mwonekano wa baadhi ya mabanda katika maonesho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Kikundi cha ngoma ya asili ya wasukuma kikitumbuiza kwenye ufunguzi wa Siku ya Mabaharia Duniani inayoadhimishwa kitaifa katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza kuanzia Alhamisi Juni 22, 2023 hadi Jumapili Juni 25, 2023.
SOMA ZAIDI HAPA

No comments:

Powered by Blogger.