LIVE STREAM ADS

Header Ads

TBS yasaini mkataba wa ushirikiano na Halmashauri za Mkoa Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Binuru Shekidere (kulia) wakisaini mkataba wa ushirikiano baina ya TBS na Halmashauri za Mkoa Mwanza.
***

Na Alex Gwido & George Binagi, Mwanza
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Ziwa limesaini mkataba wa ushirikiano na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa Mwanza, unaolenga kukaimisha majukumu ya TBS kwa Halmashauri hizo.

Mkataba huo umesainiwa Ijumaa Juni 09, 2023 ukishuhudiwa na Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa awali baina ya TBS na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini (OR- TAMISEMI).

Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Kanyeka amesema hatua ya mamlaka hiyo kukaimisha baadhi ya majukumu yake kwa Halmashauri ikiwemo ukaguzi wa ubora na usalama wa bidhaa mbalimbali itasaidia wananchi kupata huduma bora za ukaguzi.

Kanyeka amesema kupitia makubaliano hayo, maafisa wakaguzi wa halmashauri watasaidia ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazoingia sokoni ikiwemo vyakula na vipodozi na kuchukua hatua mapema kwa bidhaa ambazo hazipaswi kuwa sokoni zikiwemo bidhaa bandia na zenye kemikali zilizopigwa marufuku na hivyo kuondoa madhara yanayoweza kuwapata watumiaji.

“Tunaamini kwa sasa wananchi watapata huduma bora, kwa haraka na karibu zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo huduma ya kaguzi mbalimbali ilikuwa ikifanywa na maafisa wa TBS pekee” amesema Kanyeka.

Naye Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya amewataka Watendaji wa Halmashauri waliokasimishwa mamlaka ua ukaguzi na TBS kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kama ilivyokusudiwa na kuwaepusha kutumia bidhaa zisizopaswa kuwa sokoni.

Baada ya zoezi la kusaini mkataba huo, TBS pia imekabidhi vishikwambi kwa halmashauri zote nane za Mkoa Mwanza ambavyo vitasaidia ukusanyaji wa taarifa za kaguzi mbalimbali ili kuhakikisha bidhaa za vyakula na vipodozi zinazozalishwa ndani na nje ya nchi zinakidhi viwango kabla ya kuingizwa sokoni.

"Makubaliano haya yatasaidia ukaguzi wa bidhaa kufanyika katika maeneo mengi zaidi ambayo yalikuwa hayafikiwi kwa wakati kutokana na changamoto za kimazingira na umbali, lakini kupitia maafisa wa Halmashauri itakuwa rahisi kuyafikia maeneo yote" amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Shelembi.

Tayari TBS imesaini mkataba wa ushirikiano baina ya TBS na Halmashauri pamoja na kukabidhi vishikwambi katika Halmashauri hizo katika mikoa ya Tabora, Singida na Mwanza ambazo zoezi linaendelea katika mikoa mingine nchini lengo likiwa ni kusogeza karibu na wananchi huduma ya ukaguzi wa bidhaa mbalimbali ili kuhakikisha zinazozalishwa na kuingizwa sokoni zinazingatia usalama na ubora.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka akizungumza wakati wa zoezi la kusaini mkataba wa ushirikiano baina ya TBS na Halmashauri za Mkoa Mwanza.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Fidelica Myovella (kulia) wakionesha mkataba wa ushirikiano baada ya kuusainiwa na pande zote mbili.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Binuru Shekidere (kulia) wakibadilishana mkataba wa ushirikiano baada ya pande zote mbili kuusaini.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Sherembi (kulia) wakionesha mkataba wa makubaliano baada ya kusainiwa na pande zote mbili.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Happiness Msanga (kulia) wakibadilishana mkataba wa ushirikiano.
Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya (wa tatu kushoto) akimkabidhi kishikwambi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Sherembi (kulia) kilichotolewa na TBS kwa ajili ya kusaidia ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za ukaguzi wa bidhaa za vyakula na vipodozi.
Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya (wa tatu kushoto) akimkabidhi kishikwambi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Fidelica Myovella (kulia) kilichotolewa na TBS kwa ajili ya kusaidia ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za ukaguzi wa bidhaa za vyakula na vipodozi.
Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya (wa tatu kushoto) akimkabidhi kishikwambi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Happiness Msanga (kulia) kilichotolewa na TBS kwa ajili ya kusaidia ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za ukaguzi wa bidhaa za vyakula na vipodozi.

No comments:

Powered by Blogger.