LIVE STREAM ADS

Header Ads

SMAUJATA yaanzisha kampeni ya kutokomeza Ukatili wa Kijinsia

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Makamu Mwenyekiti wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni mkoani Singida , Wallece Shechambo akitoa elimu ya kupinga ukatili wakati walipokuwa wakishiriki shughuli ya kijamii ya ujenzi wa madarasa katika Shule Mpya ya Msingi ya Muungano Maghorofani hivi karibuni, ambapo walizindua kampeni mpya ya kuongeza mashujaa wa kupinga ukatili ijulikanayo kama 'Two by Two'

Na Dotto Mwaibale, Manyoni
Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni mkoani Singida wameanzisha kampeni ya kuongeza mashujaa kwa kila nyumba kwa ajili ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ambayo itajulikana kwa jina la Wawili kwa Wawili (Two by Two).

Akizungumza na waandishi wa habari Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Wallece Shechambo wakati walipokuwa wakishiriki shughuli ya kijamii ya ujenzi wa madarasa katika Shule Mpya ya Msingi ya Muungano Maghorofani alisema kampeni hiyo imelenga kuongeza mashujaa wa mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili katika kata hiyo na maeneo mengine yote ya wilaya ya Manyoni.

“Kampeni hii tumeipa jina la wawili kwa wawili ‘Two by Two’ yaani tutapita kila kaya iliyopo ndani ya kata yetu kutoa elimu ya kupinga ukatili na kuhamasisha watu wawili katika nyumba husika wawe mashujaa ambao nao watakwenda kwenye kaya iliyo jirani nao kutafuta mashujaa wawili hadi kila nyumba iwe na mashujaa hao,” alisema Shechambo.

Alisema kampeni hiyo itasaidia kuwa na mashujaa kila nyumba wa kupinga ukatili na kuwa kama kata yao itakuwa na kaya 10,000 basi na mashujaa watakuwa 20,000 jambo litakalo saidia kutokomeza kabisa vitendo hivyo kama sio kuvipunguza.

Shechambo alisema kampeni hiyo ya majaribio kama itafanikiwa wataisambaza katika kata zingine na kuwa kila kiongozi wa SMAUJATA wa kata hiyo ametakiwa kuwa wa kwanza kupita katika kila kaya kupata mashujaa hao wawili.

Alisema mashujaa watakao patikana kwenye kaya hizo wanaweza kuwa baba na mama, wasichana au wavulana bila kujali elimu na taaluma zao ili mradi tu waweze kupaza sauti ya kufichua vitendo vyote vya ukatili na kutoa taarifa kwenye vyombo husika kama ofisi za kata na dawati la jinsia lililopo katika vituo vya polisi na kwa maafisa ustawi wa jamii.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Mwembeni, Saluthary Naaly alisema moja ya kazi ya Mashujaa wa SMAUJATA ni kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ambapo wataweza kukutana na wananchi na kuwapa elimu hiyo ya kupinga ukatili.

Alisema kampeni hiyo ya Two by Two inakwenda kumaliza kabisa ukatili katika kata hiyo na maeneo mengine kwa kuwa kila nyumba itakuwa na shujaa wa kupinga vitendo hivyo.

Alisema kazi kubwa waliyoifanya wakati wakishiriki ujenzi wa shule hiyo ni ubebaji wa matofali, kuchota maji na kutolewa kwa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili, madhara ya ndoa za utotoni na kuwanyima watoto haki ya kupata elimu iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Wallece Shechambo.

Katibu wa SMAUJATA wa kata hiyo Sarah Yohana alisema changamoto kubwa iliyopo kwa baadhi ya wanaume ni kuwabana wake zao na kushindwa kushiriki katika mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali na kupinga ukatili.

Makamu Katibu wa SMAUJATA wa kata hiyo, Joyce Peter alisema kuna faida kubwa ya kushirikiana baina ya familia na familia katika shughuli mbalimbali ziwe za huzuni, furaha na maendeleo jambo kubwa likiwa ni kudumisha upendo.

Mjumbe wa SMAUJATA wa kata hiyo, Neema Masabuni alizungumzia kuhusu madhara yanayoweza kutokea kutokana na kutokuwepo kwa ushirikiano katika jamii na kuwa siku zote utengano ni udhaifu.

Kwa upande wake Mjumbe wa SMAUJATA wa kata hiyo, Matilda Musa alizungumzia kuhusu wajibu wa kuwa na uhusiano mzuri katika familia huku mjumbe mwenzake Zena Salimu akihimiza suala zima la kufichua vitendo vya ukatili.

Mwenyekiti wa SMAUJATA wa Kata hiyo, Hussein Kheri alitumia nafasi hiyo kuelezea umuhimu wa ujenzi wa shule hiyo na kuwa itasaidia kupunguza mlindukano wa wanafunzi katika shule ya Mwembeni yenye watoto 1772 na watoto kusoma katika mazingira bora ambapo aliipongeza Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa shule hiyo.
Mashujaa wa SMAUJATA wakiwa wamesimama kwenye Shule Mpya ya Muungano Maghorofani baada ya kushiriki ujenzi wa shule hiyo.
Muonekano wa eneo inapo jengwa shule hiyo.
Mashujaa wa SMAUJATA Kata ya Manyoni wakionesha furaha zao wakati wakiondoka kushiriki ujenzi wa shule hiyo.

No comments:

Powered by Blogger.