LIVE STREAM ADS

Header Ads

Tambo kuelekea ufunguzi wa Ligi ya Kikapu Mkoa Mwanza (MRBA) 2023/24

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wachezaji wa timu mbalimbali zinazoshiriki ligi ya mpira wa kikapu mkoani Mwanza msimu wa mwaka 2023/24 wameendelea kujifua huku kila upande ukitamba kufanya vizuri kwenye ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Jumamosi Julai 22, 2023 katika uwanja wa Mirongo jijini Mwanza majira ya saa kumi alasiri.

Wakati wachezaji wakiendelea kujiandaa katika viwanja mbalimbali ikiwemo Mirongo, Sabasaba, Mabatini na SAUT, homa ya mchezo wa ufunguzi inazidi kupamba kwani mchezo huo unazikutanisha timu za Bugando Planet dhidi ya Mwanza Eagles ambazo zilikutana msimu uliopita kwenye mchezo wa fainali na Bugando Planet kuibuka na ushindi hivyo mchezo huo utakuwa wa kisasi kwa Mwanza Eagles.

Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa Mwanza (MRBA), Sunday Mtaki amesema maandalizi ya ligi hiyo yamekamilika hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia ushindani mkali kwani ligi ya mwaka huu itakuwa na ushindani mkali baada ya wadau kujitokeza kudhamini ligi hiyo.

"Tumejiandaa vilivyo kupambana kwani hamasa ni kubwa baada ya wadau kujitokeza kudhamini ligi hii" amesema kiongozi wa timu ya CIC, Osaba Masso huku mchezaji wa timu ya Bugando Planet, Mwaijibe Ntabuli akisema wamejiandaa kumfunga yeyote ili kurudisha kombe nyumbani.

Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa Mwanza (MRBA) kimeingia makubaliano ya kushirikiana na wadau na wachezaji wa mchezo huo ambao ni Alphonce Kusekwa, Jeverico Pembe na Evans Liseki ili kuendesha ligi ya MRBA msimu wa mwaka 2023/24.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG

No comments:

Powered by Blogger.