LIVE STREAM ADS

Header Ads

Meya Sima alivalia njuga soko la Mlango Mmoja, Stendi ya Nyegezi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Zaidi ya miezi mine imepita tangu Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine afike katika soko la Mlango Moja na kukuta sehemu ya ujenzi wa vibanda 45 katika soko hilo haujakamilika na kuagiza apatiwe taarifa ya kina nini kimekwamisha ujenzi huo.

Jumanne Agosti 15, 2023 Meya Sima amefika tena katika soko hilo na kukuta hali ile ile, bado ujenzi huo haujakamilika huku bajeti iliyotengwa zaidi ya shilingi milioni 180 ikiwa imeisha, mradi haujakamilika kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Hali hiyo imemkwaza Meya Sima na kutoa muda wa siku saba kwa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza akiwemo Mhandisi, Mchumi na Mgavi kuhakikisha ujenzi huo unakamilika.

"Zaidi ya miaka miwili ujenzi haujakamilika, hii ni aibu kwetu. Tatizo tunapungukiwa uwajibikaji tunapopewa mamlaka. Mkurugenzi, Mhandisi, Mgavi na Mchumi, nawapa siku saba hadi Jumanne ijayo kazi hii iwe imeisha" amesisitiza Meya Sima.

Pia Meya Sima amekagua ukarabati wa ukumbi wa mikutabo wa ‘Gandhi Hall’ ambao ulitengewa bajeti ya shilingi milioni 200 na kuagiza kasoro zilizojitokeza kwenye ukarabati huo ikiwemo paa kuvuja kufanyiwa marekemisho.

Ziara ya Mstahiki Meya pia imetembelea mradi wa kushona nguo wa kikundi cha vijana cha ‘House Of Fashion’ kilichopokea mkopo wa shilingi milioni 28 mwaka 2021 kupitia fedha za mapato ya Halmashauri na kuagiza kikundi hicho kurejesha fedha hizo.

Mstahiki Meya aliyekuwa ameambatana na wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza amehitisha ziara yake katika mradi wa Stendi Kuu ya Mabasi Nyegezi na kueleza kuwa changamoto zilizobainika katika mradi huo ikiwemo uhaba wa maji na ukosefu wa mashine za kudhibiti ukusanyaji mapato kwenye milango ya kuingilia abiria na mabasi zinafanyiwa kazi kabla ya uzinduzi rasmi kufanyika.

Meneja wa stendi hiyo, Madelina Mtweve amesema tangu stendi hiyo ianze kufanya kazi kwa majaribio Juni 05, 2023 imesaidia upatikanaji wa mapato zaidi ya shilingi milioni 300 zilizotokana na malipo ya ushuru getini pamoja na upangishaji vyumba huku akibainisha kuwa bado maeneo mengi hayana wapangaji kutokana na gharama kubwa ambazo zinalalamikiwa na wapangaji suala ambalo Mstahiki Meya Sima amesema itafanyiwa kazi.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mwonekano wa sehemu ya soko la Mlango Mmoja ambalo halijaezekwa kwa muda mrefu na kuhatarisha mbao zilizotumika kuharibika.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine akiwa eneo la soko la Mlango Moja.
Mwonekano wa nje wa ukumbi wa 'Gandhi Hall' baada ya kufanyiwa ukarabati.
Mwonekano wa ndani wa ukumbi wa 'Gandhi Hall' baada ya kufanyiwa ukarabati.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine akikagua shughuli za kikundi cha ushonaji nguo cha 'House Of Fashion' kilichonufaika na mkopo wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Mwonekano wa stendi ya mabasi Nyegezi.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine akizungumza katika eneo la stendi ya mabasi Nyegezi.

No comments:

Powered by Blogger.