LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wagonjwa 35 wafanyiwa upasuaji wa kurekebisha sura Bugando

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Madaktari wabobezi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) jijini Mwanza kwa kushirikiana na madakitari kutoka Chuo Kikuu cha Duke kilichopo nchini Marekani wamefanikiwa kufanya upasuaji wa kurekebisha sura kwa wagonjwa 35.

Daktari Bingwa wa Upasuaji Sanifu Hospitali ya Bugando, Dkt. Francis Tegete amesema wamekuwa na kambi ya madaktari hao kutoka Marekani kwa lengo la kufanya upasuaji bobezi wa kurekebisha sura za wagonjwa zilizoharibika kutokana na ajali mbalimbali ikiwemo ya moto ambapo upasuaji huo umefanyika kwa muda wa siku tano.

Amesema kambi ya upasuaji sanifu imeshirikiana vizuri na idara ya mabingwa wa upasuaji wa pua, koo na masikio ili kuweza kufikia malengo ya Hospitali ya kuelekea kwenye upasuaji bobezi huku akiongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya afya imeamua kuwekeza juhudi kwa wataalamu wake wa ndani kwakuwaunganisha na wataalamu mbalimbali wa afya duniani ili wazidi kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa.

"Wagonjwa ambao wanakuwa na shida kwenye maeneo ya shingo, kichwani na usoni mara nyingi ni matatizo ambayo yanawafanya jamii iwanyanyapae na kushindwa kuchangamana nao, matibabu hayo ni makubwa yanahitaji utaalamu wa hali ya juu hivyo kuwa na timu hii kutoka Marekani inatusadia sisi kujijengea uwezo hatua itakayosaidia huduma hii kuenea kwa haraka hapa nchini" amesema Dkt.Tegete.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa na Mbobezi wa Upasuaji wa Kiuno na Nyonga, Dkt. Stephene Swetala amesema udaktari wa fundi sanifu ni moja ya upasuaji ambao ni adimu ambapo kwa Kanda ya Ziwa ni Hospitali ya Bugando pekee inatoa huduma hiyo ambapo kwa Tanzania kuna madaktari wachache katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Manoj Abraham ambaye ni miongoni mwa Madaktari Bingwa kutoka Duke Marekani amesema wataendelea kushirikiana kwa ukaribu na madaktari wa Bugando huku akiwasihi kuipeleka huduma hiyo mbali zaidi ikiwemo kuwafundisha vizazi vijavyo.

Naye Grace Rwechungula ambaye ni miongoni mwa waliofanyiwa upasuaji amewashukuru madaktari hao kwa kumpa huduma nzuri.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Upasuaji ukiendelea kwenye chumba cha upasuaji katika Hospital ya Bugando.
Daktari wa dawa ya usingizi Bugando, Elitristus Kaijahabi akiwa na wataalamu wenzake wakifuatilia hali ya mgonjwa wakati wa upasuaji.
Daktari Bingwa wa Upasuaji Sanifu Bugando, Dkt. Francis Tegete (katikati) akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilisha upasuaji wa kurekebisha sura kwa wagonjwa 35. Wengine ni Dave Barrett (kushoto) na Manoj Abraham (kulia) wote kutoka Duke.

No comments:

Powered by Blogger.