LIVE STREAM ADS

Header Ads

Rais Samia azindua Shule BOOST na SEQUIP

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia) na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa (kushoto) wakivuta pazia kuashia uzinduzi wa shule za awali, msingi na sekondari zilizojengwa nchi nzima kupitia Mradi wa Uimarishaji, Ufundishaji na Ujifunzaji (BOOST) na Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambayo imegharimu Sh. Bilioni 230. Uzinduzi huo umefanyia Oktoba 15, 2023 mkoani Singida.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua shule za awali, msingi na sekondari zilizojengwa nchi nzima kupitia Mradi wa Uimarishaji Ufundishaji na Ujifunzaji (BOOST) na Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambayo imegharimu Shilingi Bilioni 230.

Rais Samia amezindua Shule ya Msingi Imbele iliyopo Manispaa ya Singida na Sekondari ya Mwanamwema iliyopo Halmashauri ya Singida kwa niaba ya Shule 302 zilizojengwa nchi nzima kupitia miradi ya BOOST na SEQUIP.

Akizungumza na wananchi baada ya kuzindua miradi hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema shule hizo zimejengwa Tanzania nzima na kuwataka wazazi kuwasomesha watoto wao na kuhakikisha wanakwenda shuleni.

"Tulianza kujenga madarasa hayo kuanzia elimu ya awali tunataka kumuandaa mtoto kuanzia akiwa na miaka mitatu hadi minne ombi langu kwenu wazazi wenzangu ni kuhakikisha watoto wanakwenda shule" amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema amefurahishwa na watoto wa Shule ya Msingi Imbele wakati wakimuimbia nyimbo na hiyo imetokana na kujua matunda ya ujenzi wa shule hizo yanakwenda kuwanufaisha.

Aidha, Rais Samia amesema shule na miradi hiyo ni yetu hivyo inatakiwa kulindwa na kutunza ili iendelee kuwanufaisha watoto watakaokuwa wanasoma katika shule hizo.

Awali akisoma taarifa ya miradi hiyo Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Dkt. Elipidius Baganda amesema ujenzi wa miradi hiyo umekamilika kwa asilimia 100 na kuwa Halmashauri zote za Wilaya mkoani hapa kila moja ilipokea Sh.Milioni 493.6.

Leo Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea na ziara yake kwa kukagua barabara yenye urefu wa kilometa 59.9 inayotoka Mkiwa, Itigi hadi Nolanga mkoani Mbeya ambapo pia alifungua Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Ikungi na Mkalama.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu amesema shule hizo zimepunguza utoro kwa wanafunzi kutokana na kuwa jirani na kuwa hapo awali walikuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu hivyo alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa shule hizo.

Akizungumzia kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha Polisi cha wilaya hiyo amesema kitasaidia mji wa Ikungi kuwa salama.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi huo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akisikiliza wimbo maalumu uliokuwa ukiimbwa na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Imbele.
Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Dkt. Elipidius Baganda (kulia) akitoa taarifa ya ujenzi wa miradi hiyo mkoani Singida.
Hafla ya uzinduzi ikiendelea Shule ya Msingi Imbele iliyopo Manispaa ya Singida.
Hafla ikiendelea.
Muonekano wa moja ya darasa yaliyozinduliwa Shule ya Msingi Imbele iliyopo Manispaa ya Singida.
Shamrashamra za uzinduzi huo zikiendelea.
Uzinduzi huo ukiendelea.

No comments:

Powered by Blogger.