LIVE STREAM ADS

Header Ads

TAKUKURU Singida yaokoa zaidi ya Milioni 50

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU ) Mkoa wa Singida, Sipha Mwanjala akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwa kipindi cha Julai-Septemba 2023 katika kikao kilichofanyika Oktoba 27, 2023.
Kikao na waandishi wa habari na maafisa wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, kikifanyika.
Kikao kikiendelea.

Na Dotto Mwaibale, Singida
Taasi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imeokoa Sh. 54,087,750.58 zilizotokana na wazabuni kutowasilisha kodi ya zuio Mamlaka ya Mapato,Tanzania (TRA) na kupeleka vifaa pungufu katika miradi mbalimbali.

Hayo yamebainishwa Oktoba 27, 2023 na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida Sipha Mwanjala wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwa kipindi cha Julai-Septemba 2023.

Ameema TAKUKURU Mkoa wa Singida kwa kipindi cha Julai –Septemba 2023 kwa upande wa uzuiaji rushwa walifuatilia utekelezaji wa miradi kumi na tatu yenye thamani ya zaidi Sh.Bilioni 5 katika sekta ya Elimu na Barabara na kuwa ilijumuisha miradi ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa taifa kwa fedha zilizotolewa na Serikali Kuu.

Amesema miradi mitatu iliyofuatiliwa yenye thamani ya Sh. Bilioni1.4 ilikutwa na mapungufu mbalimbali ambapo walitoa ushauri ili kukabiliana na mapungufu hayo. Ametaja baadhi ya mapungufu hayo ni kupeleka vifaa pungufu katika miradi tofauti na madai aliyowasilisha au fedha alizolipwa.

Akizungumzia kuhusu chambuzi za mifumo amesema katika kipindi tajwa TAKUKURU ilifanya chambuzi saba za mifumo ili kubaini mianya ya rushwa iliyopo katika maeneo hayo na kisha kushauri namna ya kuiziba na kuwa Warsha saba zilifanyika kwa ajili ya kujadili mianya ya rushwa
iliyobainika katika chambuzi zilizofanyika na kuweka mikakati ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika.

Aidha, Mwanjala amesema TAKUKURU Mkoa wa Singida iliendelea na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa kufanya vikao 18 na wadau katika kata 18 ambapo wadau waliibua kero 175.

Amesema kero zilizotatuliwa mpaka sasa ni 125 na kero 50 zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.

Akielezea upande wa elimu kwa umma alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida imewaongezea wananchi uelewa wa masuala ya rushwa kwa kufanya Semina 34 kwenye makundi mbalimbali
wakiwemo watumishi wa umma.

Amesema pia walifanya mikutano ya hadhara 17, maonesho 7, kutembelea na kuimarisha klabu za wapingarushwa 43 katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Akizungumzia suala la uchunguzi na mashitaka alisema malalamiko 76 yalipokelewa, ambapo malalamiko 52 yalihusu vitendo vya rushwa na malalamiko 24 hayakuhusu rushwa.

Amesema malalamiko 52 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali na malalamiko 24 ambayo hayahusiani na rushwa walalamikaji walipewa ushauri.

Amesema katika kipindi hicho kesi 10 zilifunguliwa mahakamani, kesi 13 ziliamuliwa na kupata ushindi wa kesi 8.

Akizungumzia mikakati ya utendaji kazi waliojiwekea kwa robo ya pili ya mwaka 2023/ 2024 ya kuanzia mwezi ni kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali, zinazoelekezwa Mkoa wa Singida kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 Pia kuendelea kuwaongezea uelewa wananchi kuhusiana na masuala ya rushwa ili wananchi washiriki kikamilifu kuzuia vitendo hivyo hasa katika miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo yao, kuendelea na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU – Rafiki.

Mwanjala alitoa wito kwa kusema kuwa TAKUKURU Mkoa wa Singida inatoa RAI kwa wananchi wote kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu kuzuia vitendo vya rushwa vinavyotokea katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za kijamii. Pia, kuzuia vitendo hivyo hasa
katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao,na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kufika Ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Singida na Wilaya za Iramba, Ikungi, Mkalama na Manyoni.

Mwanjala alitaja njia nyingine ya kutoa taarifa hizo ni kupiga simu ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa na wakuu wa TAKUKURU wa Wilaya kwa namba RBC –Singida 0738150208, DBC -Mkalama 0738150 212, DBC - Ikungi 0738150213, DBC -Iramba 0738150 210 na DBC - Manyoni 0738150 211 na akaomba wananchi kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani.

No comments:

Powered by Blogger.