LIVE STREAM ADS

Header Ads

Madiwani washangaa mradi wa bilioni 12 kutokamilika

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Jumanne Mlagaza akiongoza kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza cha mwaka wa fedha 2023/2024 kilichoketi leo Novemba 03, 2023.

Na Dotto Mwaibale, Manyoni
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, limesikitishwa na Wakala wa Usambazaji Maji na usafi wa mazingira (RUWASA) wilayani humo kutokamilisha mradi mkubwa maji ujulikanao kama Kintiku Lusilile unaolenga kuhudumia vijiji 11 unaogharimu kiasi cha Sh.Bilioni 12.

Madiwani hao wametoa masikitiko hayo katika kikao cha kawaida cha baraza hilo cha robo ya kwanza cha mwaka wa fedha 2023/2024 wakati wakijadili taarifa ya RUWASA.

Katika kikao hicho cha madiwani kilicho hudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Dk. Pius Chaya wamekashangazwa mradi huo kutokamilika kama mkataba ulivyosainiwa ambapo ilitakiwa kazi ya ujenzi wa mradi huo iwe imekamilika ifikapo mwezi huu wa Novemba ambapo umesogezwa mbele hadi Januari 2024.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Jumanne Mlagaza akiongoza kikao hicho,amewataka madiwani kusimamia vyema miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miradi hiyo inakidhi thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo.

“Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi hii fuatilieni kwa ukaribu kwani kumekuwa na udanganyifu kwenye baadhi ya maeneo ambapo mara kadhaa miradi hukamamilika na kukabidhiwa ikiwa haijakidhi vigezo pamoja na thamani halisi,” amesema Mlagaza.

Aidha baraza hilo la madiwani limemfuta kazi Muuguzi Msaidizi, Atieno Otieno kwa sababu za utoro kazini.

Akitoa taarifa hiyo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jumanne Mlagaza amesema baraza hilo limefikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mfanyakazi huyo aliyekuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya hiyo ameenda kinyume na sheria.

"Kwa mujibu wa sheria mtu anapokosekana siku tano katika kituo chake cha kazi bila ya kuwepo kwa taarifa yoyote anakuwa amekiuka mashariti ,hivyo kuanzia leo kikao hiki cha madiwani kimeridhia kumfukuza kazi na kuanzia sasa Atieno sio mfanyakazi wa halmashauri hii” amesema Mlagaza.
Kikao kikiendelea.
Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Dk. Pius Chaya, akichangia jambo kwenye kikao hicho.Kulia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni, Jumanne Ismail.
Uchangiaji ukiendelea kwenye kikao hicho.
Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa kikao hicho.
Madiwani wakiwa kwenye kikao hicho.

No comments:

Powered by Blogger.