LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mafanikio ya mradi wa ELCAP mkoani Singida

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga akifunga kikao kazi cha kutathimini utekelezaji wa mradi wa ELCAP wa miaka mitano ulioanza Septemba 20, 2021 ambao unatarajia kumalizika Mwezi Juni, 2026/ unao tekelezwa na Shirika la SEMA kwa kushirikiana na Shirika la Stromme Foundation Tanzania.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Shirika lisilo la kiserikali la Sustainable Environment Management Action (SEMA) lenye makao yake makuu mkoani Singida kwa kushirikiana na Shirika la Stromme Foundation Tanzania kupitia mradi wa Kilimo Biashara wa ELCAP katika kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wa mradi huo wamepata mafanikio makubwa ya uongezaji uzalishaji wa mazao kwa kutoa elimu za teknolojia mbalimbali za kilimo.

Mkurugenzi wa SEMA, Ivo Manyaku akizungumza Novemba 07, 2023 kwenye kikao kazi cha kutathimini utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitano ulioanza Septemba 20, 2021 ambao unatarajia kumalizika mwezi Juni, 2026 amesema umekuwa na mafanikio makubwa kwa wakulima.

Amesema lengo la mradi huo ni kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha kwa ubora zaidi na kupata mazao mengi katika eneo dogo.

Manyaku amesema mradi huo ni mahususi kwa vijana na wanawake na ni muendelezo wa vikundi vilivyokuwa vikitumika katika mradi wa awali wa kuweka na kukopa na sasa wanawatoa katika eneo hilo na kuwaingiza kwenye uzalishaji wenye tija na kuongeza thamani kupitia mazao ya kilimo ambayo ni mahindi, alizeti, mtama na mbaazi.

Aidha, Manyaku amesema kupitia mradi huo wamefanikiwa kuwatafutia wakulima masoko kwa kuwaunganisha na wadau mbalimbali na wafanyabiashara .

Ametaja mafanikio mengine kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo wakulima walikuwa wakipata magunia ya mahindi kati ya sita hadi saba kwa heka moja lakini sasa wanapata magunia 15 hadi 20 na akamtaja mmoja wa wakulima hao kutoka Wilaya ya Ikungi kuwa alipata magunia 10 katika nusu heka.

Amesema lengo la mradi huo ni kuwafikia wakulima 6000 na kati ya hao asilimia 40 wawe vijana na asilimia mbili watu wenye ulemavu na kuwa umejikita kuhakikisha kuwa teknolojia wanazo wapa zinaendelea kuwasaidia wakulima hata baada ya mradi huo kumalizika.

Amesema pamoja na kuwa na lengo la kuwafikia wakulima 6000 lakini kwa kupitia mnyororo wa thamani wanatamani kuwafikia wakulima 10,000 katika wilaya ambazo unafanyika mradi huo ambazo ni Iramba, Ikungi na Manyoni na kuwa gharama ya mradi huo ni Sh.Bilioni 4.5.

Amesema mradi huo unatekelezwa na SEMA kwa kushirikiana na Stromme Foundation na nchi ya Norway pamoja na washirika wao wa kimkakati, NGI, CSFS na NMBU ambao wanawawezesha kuwapa teknolojia.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga amepongeza mashirika hayo kwa kuusaidia Mkoa wa Singida katika sekta ya kilimo.

“Katika mradi huu ni Singida peke yake ndiyo inasaidiwa kuhakikisha inaboresha kilimo ili kuongeza uzalishaji na hasa kwa kutumia teknolojia inayokwenda kuhifadhi maji katika mashamba yetu na kurutubisha ardhi na kuboresha maisha ya familia zetu” amesema Mganga.

Amesema kwa kuwa mradi huo una walenga wakulima wadogo hasa wanawake na vijana katika wilaya za Ikungi, Iramba na Manyoni anaamini kutokana na kuwa wepesi wa kuelewa watakwenda kuleta mabadiliko chanya kwenye familia zao kwani wakiwezeshwa kupata mikopo na mbegu bora mashamba yao yanakwenda kuwa dhahabu katika Mkoa wa Singida.

Pamoja na mambo mengine ameshauri mradi huo uweze kufika mpaka shule za msingi na sekondari.kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti Wizara ya Kilimo, Mohammed Chikawe ameyashukuru mashirika hayo kwa kuungamkono jitihada za Serikali katika sekta ya kilimo mkoani hapa na kueleza mradi huo unatekelezwa vizuri ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau hao wa maendeleo kuusambaza na kwenye mikoa mingine ili nayo iweze kupata teknolojia hiyo ya uzalishaji wa mazao na kuongeza thamani pamoja na kuwatafutia masoko kama ilivyofanya katika Mkoa wa Singida.

Wajasiriamali na wanufaika wa mradi huo Anna Ntandu kutoka Wilaya ya Ikungi na Rehema Mwaliwa kutoka Kata ya Iseke wilayani Ikungi wameyashukuru mashirika hayo kwa kuwapa mafunzo ya kilimo biashara ambayo yamewakomboa kiuchumi na kuweza kujikimu kimaisha na kusomesha watoto wao.

“Changamoto kubwa tuliyonayo ni vifaa vya kufanyia kazi, mtaji na masoko ya uhakika kwa mfano mimi nalazimika kutumia sufuria kwa ajili ya kuoka mkate badala ya oveni naomba tunapo hitimu mafunzo tuwe tunawezeshwa vifaa hivyo hata kwa kukopeshwa” amesema Mwaliwa.
Mkurugenzi wa SEMA, Ivo Manyaku akitoa taarifa ya mradi huo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti Wizara ya Kilimo, Mohammed Chikawe akizungumza kwenye kikao hicho.
Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa SEMA, Daniel Chacha akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwakilishi wa Shirika la CSFS kutoka Zambia, Gibson Simusokwe akitoa mada kwenye kikao hicho.
Mwakilishi kutoka Shirika la NGI la , Nchini Norway Profesa Gerard Cornelissen akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwakilishi wa Shirika la NMBU kutoka Nchini Norway, Profesa. Jan Mulder akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Mratibu wa miradi wa ELCAP, Alunas Maxwell akiongoza kikao kazi hicho.
Meneja wa Miradi ya Stromme Foundation Tanzania , Doreen Matekele akizungumza kwenye kikao hicho.
Mjasiriamali mnufaika na mradi huo, Anna Ntandu akiyashukuru mashirika hayo kwa kuwapa mafunzo ya kilimo biashara.
Mnufaika na mafunzo ya kilimo biashara, kutoka Kata ya Iseke wilayani Ikungi, Rehema Mwaliwa akitoa shukurani baada ya kupata mafunzo hayo.
Washiriki kutoka Stromme Foundation Kampala Uganda wakiwa kwenye kikao kazi hicho.
Kikao kikiendelea.
Kikao kazi kikiendelea.
Taswira ya kikao kazi hixmafunzo hicho.
Mgeni rasmi wa kufunga kikao hicho, Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga akikagua bidhaa za wajasiriamali walionufaika na mradi huo.
Picha ya pamoja na wadau wa mradi huo kutoka Norway.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Shirika la SEMA.

No comments:

Powered by Blogger.