LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la Teens Corridor latambulisha mradi wa Ujuzi ni Mchongo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Teens Corridor lenye ofisi zake Kata ya Kawekamo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza limetambulisha mradi wa Ujuzi ni Mchongo, unaolenga kuwajengea vijana ujuzi wa sanaa ya uchoraji na masoko ili kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza Jumamosi Novemba 11, 2023 wakati wa hafla fupi ya kuutambulisha mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Sophia Nshushi amesema mradi huo wa majaribio unatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miezi mitatu.

"Mradi unalenga kuwawezesha vijana kukuza vipaji vyao katika eneo la uchoraji ambapo tuna makundi mawili. Kundi la kwanza ni vijana ambao tayari wana ujuzi wa kuchora ambapo tunawawezesha kupata masoko ndani na nje ya Tanzania" amesema Nshushi na kuongeza;

"Kundi la pili ni vijana ambao wana vipaji na wanapenda kuchora ila hawana ujuzi hivyo tunawapa ujuzi zaidi" amesema Shushi akibainisha kuwa mbali na vijana pia watoto wenye vipaji vya uchoraji watanufaika na mradi huo.

Pia Nshushi amebaisha kuwa tayari vijana 10 wamejiunga na mafunzo ya uchoraji yanayotolewa kupitia mradi huo ambapo matarajio ni kuona vijana wengi zaidi wenye vipaji vya uchoraji wakijiunga na mafunzo hayo.

"Tuna vijana ambao wamehitimu vyuo lakini kutokana na changamoto ya ajira wametumia ujuzi wa sanaa ya uchoraji kujiajiri na sasa wanajipatia kipato na kuondokana na utegemezi katika jamii" amesema Nshushi.

Naye mmoja wa vijana wachoraji kupitia mradi huo wa Ujuzi ni Mchongo, Thomas Gabriel amesema sanaa ya uchoraji imewasaidia kujipatia kipato na kujiepusha na vishawishi vya kujiingiza kwenye makundi hatarishi katika jamii.

Baadhi ya watoto ambao tayari wamejiunga na mradi huo ni Caroline Casto, Angel Renatus na Eflatha Boniphace. Watoto hao wamesema wanavutiwa na sanaa ya uchoraji kwa kuwa wanapata fursa ya kuelezea hisia zao kupitia michoro ambapo matarajio ni kuwa wachoraji maarufu na kujipatia kipato.

Shirika la 'Teens Corridor Organization' ni shirika la vijana lenge malengo makuu matatu ambayo ni kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kujipatia kipato, elimu ya afya ya uzazi na kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wenza.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Teens Corridor, Sophia Nshushi (kulia) akizungumza kwenye hafla ya kuutambulisha mradi wa ujuzi ni mchongo. 
Kushoto ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Kawekamo B, Moshi Malima eneo zilipo ofisi za shirika la Teens Corridor, ambapo amewahimiza vijana kuzingatia maadili wakati wa utekelezaji wa mradi huo na kwanza Serikali ya Mtaa huo itawapa ushirikiano wa kutosha.
Mjumbe wa bodi ya shirika la Teens Corridor, Astar Masawe akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa ujuzi ni mchongo unaolena kuwajengea vijana ujuzi wa uchoraji ili kuwasaidia kujipatia kipato.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Teens Corridor, Sophia Nshushi (kulia) akiwa na viongozi na wadau mbalimbali waliofika katika ofisi za shirika hilo kwa ajili ya uzinduzi wa mradi wa ujuzi ni mchongo.
Angel Renatus (kushoto) na Caroline Casto (kulia) wakijifunza uchoraji.
Darasa la kufundisha uchoraji kupitia mradi wa ujuzi ni mchongo unaotekelezwa na shirika la Teens Corridor la jijini Mwanza.
Darasa la kufundisha uchoraji kupitia mradi wa ujuzi ni mchongo unaotekelezwa na shirika la Teens Corridor la jijini Mwanza.
Darasa la kufundisha uchoraji kupitia mradi wa ujuzi ni mchongo unaotekelezwa na shirika la Teens Corridor la jijini Mwanza.
Mmoja wa wadau akijipatia picha iliyochorwa kupitia mradi wa ujuzi ni mchongo.
Vijana wachoraji ambao pia wanafundisha vijana wenzao kuchora kupitia mradi wa ujuzi ni mchongo unaotekelezwa na shirika la Teens Corridor.
Mmoja wa vijana wachoraji, Thomas Gabriel (katikati) akitoa ufafanuzi wa picha mbalimbali anazochora ikiwemo za watu mashuhuli, wanyama, mimea na viumbe mbalimbali.
Wadau wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa hafla ya kuutambulisha mradi wa ujuzi ni mchongo unaotekelezwa na shirika la Teens Corridor unaolenga kuwajengea ujuzi vijana katika sanaa ya uchoraji pamoja na kuwasaidia kujitangaza ili kutanua wigo wa masoko ndani na nje ya Tanzania.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

No comments:

Powered by Blogger.