LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kongamano la kuwajengea uwezo wanawake lafanyika Nyamagana

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wilaya ya Nyamagana imeadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kuwajengea uwezo wanawake kupitia kongamano lililowasaidia kuzitambua fursa za kijamii na kiuchumi zilizopo mkoani Mwanza hatua itakayowasaidia kujikwamua kimaendeleo.

Kongamano hilo lililoambatana na mada za elimu mbalimbali ikiwemo mikopo, ukatili, ujasiriamali na afya limefanyika Machi 06, 2024 katika uwanja wa michezo Nyamagana jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa kufungua kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi alisema katika maisha ya binadamu inatakiwa kuwepo na msukomo utakaomuwezesha kufanya mabadiliko ya kiuchumi ndiyo maana wamewajengea uwezo wanawake ili waweze kuongeza chachu ya kusukuma maendeleo kwenye jamii.

Alieleza kuwa dhamira ya Serikali ya Tanzania ni kuwekeza nguvu nyingi kwa wanawake ikiwemo kuwawezesha kushika nyanja mbalimbali za kisasa, kiuchumi na kijamii.

"Nitoe wito kwa wanawake wa Wilaya ya Nyamagana jitokezeni kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya Mtaa, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla" alisema Makilagi akiwahamasisha wananwake kushiriki uchaguzi mdogo 2024 na uchaguzi mkuu 2024.

Aidha alisema kwa sasa wanawake wana uwezo wa kumiliki ardhi, mali, kuendesha biashara tofauti na zamani ambapo walikuwa hawawezi kumiliki chochote na hivyo kuwahimiza kutumia fursa hiyo vyema.

Makilagi aliwakumbusha wazazi pamoja na majukumu ya utafutaji wa riziki, waweke utaratibu kwenye familia wa kufuatilia mienendo ya masomo ya watoto wao pindi wanaporudi nyumbani.
Akitoa mada ya uwezeshaji wanawake kiuchumi na urasimishaji wa biashara, Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mariam Mdesa alisema wanawake wanapoanzisha vikundi wahakikishe wanavisajili ili iwe rahisi kukopesheka kwenye taasisi mbalimbali za kifedha.

Alieleza kuwa vikundi ni fursa na fursa nyingi zinazotolewa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza zinapitia kwenye vikundi hivyo wanawake wajiunge kwenye vikundi hivyo ili wapate fedha za kufanyia biashara.

"Halmashauri ya Jiji la Mwanza inatoa mikopo inayotokana na mapato ya ndani na ili kikundi kipewe mkopo lazima kiwe kimesajiliwa pamoja na mradi unaoendeshwa na wanakikundi" alisema Mdesa.

Kwa upande wake Meneja Mahusiano benki ya CRDB Kanda ya Ziwa, Joyce Maluba alisema benki hiyo imeanzisha taasisi ya CRDB Foundation kwa ajili ya kuwainua wanamke kupitia mikopo ambayo haina riba wala dhamana.

"Kitu cha msingi ni uaminifu hivyo niwaombe sana wanawake wote nchini, changamkieni fursa hii kwa kufika kwenye matawi ya CRDB kwa ajili ya kufungua akaunti za imbeju na mfuatilie mikopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi, tunaanza kutoa mikopo kuanzia laki mbili hadi milioni 30" alisema Maluba.
Baadhi ya wanawake walioshirikikongamano hilo wakicheza muziki.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.