LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mkurugenzi Jiji la Mwanza atoa siku nne kwa wafanyabishara

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu wafanyabiashara wanaodaiwa kodi kulipa kodi hiyo ndani ya siku nne kuanzia leo Alhamisi Mei 02, 2024.


Na Hellen Mtereko, Mwanza
Halmashauri ya Jiji la Mwanza imetoa siku nne kuanzia Alhamisi Mei 02 hadi Jumapili Mei 05,2024 kwa wafanyabiashara jijini humo kulipa kwa hiari ushuru, kodi na ada mbalimbali wanazodaiwa.

Siku hizo zimetolewa baada ya uongozi wa Halmashauri hiyo kuona wafanyabiashara hao wakisuasua katika ulipaji wa tozo hizo licha ya jitihada mbalimbali ambazo zimefanyika ikiwemo kutumia watendaji wa mitaa na magari ya matangazo kuwakumbusha na kuhamasisha lakini hawakufaya hivyo.

Kauli hiyo imetolewa Alhamisi Mei 02, 2024 na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Wakili Kiomoni Kibamba wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amesema kutokana na bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka 2022/23, wanatakiwa kukusanya takribani bilioni tano kwenye vyanzo mbalimbali ambapo kodi hizo zinaiwezesha Halmashauri kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa mujibu wa sheria.

"Mwaka wa fedha unaisha Juni 30 mwaka huu katika miezi hii miwili, tumejipanga kuhakikisha kila Senti inayopaswa kukusanywa inakusanywa pasipo kupoteza hata senti moja, hivyo wafanyabiashara msisubiri hadi tuchukue hatua ambazo hazitawafurahisha" amesema Wakili Kibamba.

Aidha ametoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanalipia kodi zote kwenye mifumo ya kielektroniki ili kuepuka usumbufu utakaoweza kujitokeza ikiwemo ya kutotambulika kwa malipo yao.

Katika hatua nyingine Kibamba amewataka wananchi kuepuka ujenzi holela na kuwahimiza kabla ya kuanza shughuli za ujenzi ni vyema kupata kibali kutoka Halmashauri hatua itakayowaepusha kuingia katika hasara ya kubomolewa maeneo waliyojenga kiholela.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba akionesha nyaraka mbalimbali zenye orodha ya majina ya wafanyabiashara pamoja na makampuni ya maegesho ambao hawajalipa kodi ambapo amewataka kulipa madeni yao ndani ya siku nne kuanzia leo Alhamisi Mei 02, 2024.

No comments:

Powered by Blogger.