LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waandishi wa habari wahimizwa kuibeba ajenda ya mazingira

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
    Waandishi wa habari mkoani Mwanza wamehimizwa kuibeba kwa vitendo ajenda ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kutumia vyombo vya habari kuelimisha jamii hatua itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Rai hiyo imetolewa Jumanne Mei 07, 2024 na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza (MPC), Edwin Soko wakati akizungumza kwenye kongamano la maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari lililofanyika katika Chuo Kikuu cha SAUT.

Soko amesema changamoto ya uharibifu wa mazingira imesababisha mabadiliko ya tabianchi na athari zake tayari zimeanza kuonekana ambazo ni pamoja na mafuriko katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Amesema kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ambayo ni uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, imelenga kutoa msukumo kwa waanishi wa habari kubeba wajibu wa kuelimisha jamii kuhusu utunzaji mazingira.

Katika hatua nyingine, Soko amesema uhuru kwa waandishi wa habari nchini umeongezeka kiasi cha kuifanya Tanzania kushika nafasi ya 97 kutoka nafasi ya 143 japo changamoto za kisheria bado zipo na jitihada za kuhimiza zifanyiwe marekebisho bado zinaendelea.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SAUT, Prof. Costa Ricky Mahalu amewataka waandishi wa habari kutumia weledi wao kuleta mabadiliko katika jamii hususani katika masuala ya utunzaji mazingira akisema jamii ina imani kubwa na kazi inayofanywa na waandishi wa habari.

Naye Afisa Taaluma kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Joviter Mombeki amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa waandishi wa habari hivyo matarajio ni kuona wakifanya kazi kwa weledi kuelimisha jamii katika sekta mbalimbali ikiwemo mazingira huku wakijiepusha na habari potofu katika jamii.

Mwanafunzi wa masomo ya uandishi wa habari Chuo Kikuu SAUT, Fidelis Seleman amesema uandishi wa habari za mazingira unasaidia jamii kupata elimu na hatua salama za kuchukua wakati wa majanga kama mafuriko ama kimbuka na kutoa rai kwa wananchi kutambua umuhimu wa habari hizo.

Siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani huadhimishwa kila mwaka Mei 03 ambapo kitaifa ilifanyika mkoani Dodoma ambapo kwa Mkoa Mwanza imefanyika Mei 07, 204 kwa ushirikiano baina ya MPC na Chuo Kikuu SAUT.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko akizungumza kwenye kongamano hilo.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali akizungumza kwenye kongamano hilo na kueleza kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikiwajengea uwezo waandishi wa habari kutimiza majukumu yao kwa weledi.
Mwanafunzi wa masomo ya uandishi wa habari Chuo Kikuu SAUT, Fidelis Seleman akizungumza kwenye kongamano hilo.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SAUT, Prof. Costa Ricky Mahalu akizungumza na waandishi wa habari.
Mkuu wa Idara ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma Chuo Kikuu SAUT, Dkt. Okechukwu Chukwuma akizungumza na waandishi wa habari akisisitiza kwamba waandishi wa habari wanao wajibu wa kuhakikisha jamii inachukua hatua kuhifadhi mazingira.
Wanafunzi wa uandishi wa habari Chuo Kikuu SAUT wakifuatilia kongamano hilo.

No comments:

Powered by Blogger.