LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Nyamagana asisitiza utoaji chakula kwa wanafunzi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi amewaagiza Watendaji wa Mitaa na Kata kuendelea kuimarisha utekelezaji wa mikakati ya utoaji chakula kwa wanafunzi ili kuhakikisha shule zote za msingi na sekondari zinatoa huduma hiyo.

Makilagi ametoa agizo hilo Jumatatu Mei 06, 2024 wakati akizungumza na Watendaji wa Mitaa na Kata katika kikao cha lishe cha robo ya tau ya mwaka wa bajeti wa 2023/24 kilicholenga kupeana taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe wilayani humo.

Amewataka kutoa elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa lishe kwa wanafunzi na kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha huduma ya chakula inatolewa kwa wanafunzi hatua itakayosaidia wanafunzi kuzingatia vyema masomo darasani.

Makilagi pia amewakumbusha viongozi hao kusimamia vyema utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii kila mwezi kupitia siku ya lishe ya jamii ya mtaa hatua itakayosaidia wananchi ujifunza namna rahisi ya kuandaa chakula cha lishe ili kupambana na udumavu/ utapiamlo hususani kwa watoto.

Katika hatua nyingine, Makilagi amekabidhi vyeti vya pongezi vilivyotolewa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa Kata za Luchelele, Mahina, Kishiri na Butimba kwa kusimamia vyema afua za lishe ikiwemo kutoea elimu kwa jamii na chakula kwa wanafunzi ambapo ameagiza robo ya nne ijayo vyeti hivyo viambatane na zawadi ya fedha ili kutoa hamasa zaidi.

Mkuu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Dkt. Sebastian Pima amesema hali mbaya ya lishe ikiwemo kula aina moja ya chakula inaweza kusababisha utapiamlo na udumavu na hivyo kusababisha taifa kuwa na wananchi ambao hawawezi kuwa na tija kiuchumi.

Dkt. Pima amesema utekelezaji wa mkataba wa lishe utasaidia elimu kutolewa kwa jamii kuhusu namna bora na rahisi ya kuandaa chakula chenye lishe, hatua itakayosaidia jamii kuondokana na changamoto ya utapiamlo.

Katika kuhakikisha jamii inapata elimu, Wilaya ya Nyamagana imeandaa kongamano la siku ya wanafamilia litakalofanyika katika Kata ya Mabatini Mei 20, 2024 ili kutoa elimu na maonesho ya namna bora ya kuandaa chakula cha lishe.
 Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (kushoto) akikabidhi cheti cha pokezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (hayuko pichani) kwa kutoa fedha za lishe. Cheti hicho kimepokelewa kwa niaba yake na Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Erick Mvati (kulia).
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (kushoto) akikabidhi vyeti vya pongezi kwa Kata zilizofanya vizuri katika afya za mkataba wa lishe.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (kushoto) akikabidhi vyeti vya pongezi kwa Kata zilizofanya vizuri katika afya za mkataba wa lishe.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (kushoto) akikabidhi vyeti vya pongezi kwa Kata zilizofanya vizuri katika afya za mkataba wa lishe.
Katika hatua nyingine, DC Makilagi ameagiza Halmashauri ya Jiji la Mwanza katika bajeti ijayo ya mwaka 2024/25 kuandaa bajeti ya kuunga mkono jitihada za wazazi kuchangia chakula kwa wanafunzi akisema, "wazazi wakileta unga wa uji, basi Serikali ichangie sukari au maziwa, pia tuje na mpango wa kutafuta mashamba na kulima mazao ya chakula kwa ajili ya wanafunzi".
Tazama BMG TV hapa chini
SOMA PIA>>> HABARI ZAIDI HAPA

No comments:

Powered by Blogger.