LIVE STREAM ADS

Header Ads

UTPC yashiriki Maonesho ya Kimataifa Idodomia, DC Bahi atoa kongole

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Gift Msuya ameupongeza umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania kwa kuenea nchi nzima kupitia Klabu zake 28 za Waandishi wa Habari.

Msuya ametoa pongezi hizo za dhati kwa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania tarehe 20 Juni 2024 katika ufunguzi wa maonesho ya Kimataifa ya fursa za uwekezaji, utalii, michezo na utamaduni, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

Akiwa katika banda hilo lililopambwa kwa uzuri na mabango, vipeperushi, vitabu, majarida na vijitabu vinavyoeleza maana na shughuli zinazotekelezwa na UTPC alisema, "Nimekuwa nikifuatilia UTPC kwa miaka mingi na ninaona kazi zenu zenye mchango mkubwa kama sekta ya habari na mawasiliano kupitia waandishi wenu katika Klabu zote 28 nchini Tanzania. Uadilifu weu katika uandishi wa tasnia ya uandishi wa habari ni rasilimali muhimu sana kwa Serikali yetu na nchi yetu.

Aliongeza, "Jana tu nilikuwa nikifuatilia mkutano wenu na Rais Samia Suluhu Hassan katika Kongamani la Maendeleo ya Sekta ya Habari. Kwa kweli mnafanya kazi nzuri sana kwa Taifa letu".

Naye kwa upande wake Afisa Habari, Mawasiliano na Uratibu UTPC, Rose Mwanga alieleza shughuli zinazotekelezwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania ikiwa ni pamoja na miradi mbalimbali ikiwemo "Mtoto Kwanza" ambapo kwa kushirikiana na Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM), na mradi wa kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira rafiki na kuchochea uhuru wa kujieleza.

Aliongeza kuwa, "Serikali ni wadau wetu wakubwa hasa kupitia Wizara yetu ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya Waziri mwenye dhamana Nape Nauye".

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Dodoma waliotembelea banda la Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania, kwa nyakati tofauti walieleza namna walivyopendezwa na maelezo ya shughuli zinazofanywa na umoja huo.

"Mimi ni mwandishi wa habari lakini nilikuwa sijajiunga na Klabu yoyote ya Uandishi, kwa sasa nahitaji kujiunga, naomba utaratibu wa jinsi ya kujiunga" alisema David Lameck, mmoja wa wadau waliotembelea Banda la UTPC.

"Nimetembelea mabanda mengi katika maonesho haya, lakini hili lina upekee sana, hii ni taasisi ya kihabari pekee, hongereni sana" alisema Happy Mkunwa.

Maonesho haya ya kimataifa ya fursa za uwekezaji, utalii, michezo na utamaduni yalianza tarehe 18 Juni 2024 na yatahitimishwa tarehe 22 Juni 2024.

Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania ni asasi mwamvuli wa Klabu 28 za Waandishi wa Habari nchi nzima ikiwa na wanachama zaidi ya 1,500.

No comments:

Powered by Blogger.