LIVE STREAM ADS

Header Ads

UWADOMAMI wasaini makubaliano na wasafirishaji mizigo minadani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Umoja wa wafanyabishara wadogo katika masoko na minada mkoani Mwanza (UWADOMAMI), umesaini makubaliano na wasafirishaji wanne kwa ajili ya kusafirisha mizigo katika masoko na minada.

Makubaliano hayo ya miaka minne yamesainiwa Jumatatu Juni 03,2024 katika ofisi za UWADOMAMI zilizopo Buhongwa jijini Mwanza, yakihusisha minada iliyopo katika Wilaya za Nyamagana, Ilemela, Magu na Sengerema.

Katibu Mkuu wa UWADOMAMI mkoani Mwanza, Davis Philipo amewataja wasafirishaji waliokidhi vigezo na kupewa ridhaa ya kusafirisha mizigo katika masoko na minada ni Mambo ya Chinga, Makusanya, Mpaji ni Mungu na Miss Meru.

Naye Mwenyekiti wa UWADOMAMI Mkoa Mwanza, Justine Sagara amewataka wasafirishaji hao kuzingatia makubaliano ya mkataba huo na kuepuka kuingiliana njia huku akiahidi kuwa chama hicho pia kitahakikisha wanafanya kazi bila kuingiliwa na wasafirishaji wasio na kibali.

Akizungumza kwa niaba ya wasafirishaji wenzake, mmiliki wa malori ya Makusanya, Daud Makusanya amesema wamejipanga kusafirisha mizigo ya wafanyabishara wadogo katika masoko na minada ili kuwawezesha kufanya biashara zao ambapo ametumia fursa hiyo kuomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara inayoelekea kwenye masoko na minada.

"Awali kulikuwa na changamoto kwenye kusafirisha mizigo kwenye masoko na minada ikiwemo kuingiliwa na wenye bajaji za mizigo lakini baada ya makubaliano haya, tunaamini sasa zitakwisha" amesema Esther Palanjo kutoka kampuni ya Miss Meru.

Makubaliano hayo yameshuhudiwa na Mwanasheria, Nzaniye Karubutse ambaye ametoa rai kwa pande zote mbili kuyaheshimu kwani kushindwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha yavunjike na hatua za kisheria kuchukuliwa.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mwenyekiti wa UWADOMAMI Mkoa Mwanza, Justine Sagala akizungumza wakati wa kusaini makubaliano na wasafirishaji wa mizigo kwenye masoko na minada.
Katibu Mkuu UWADOMAMI Mkoa Mwanza, Davis Philipo akizungumza wakati wa kusaini makubaliano na wasafirishaji wa mizigo kwenye masoko na minada.
Zoezi la kusaini makubaliano baina ya UWADOMAMI na wamiliki wa malori kwa ajili ya kusafirisha mizigo kwenye masoko na minada.
Viongozi wa UWADOMAMI ngazi ya Wilaya wakisoma makubaliano baina ya UWADOMAMI na wasafirishaji mizigo kwenye masoko na minada.
Viongozi wa UWADOMAMI ngazi ya Wilaya wakisoma makubaliano baina ya UWADOMAMI na wasafirishaji mizigo kwenye masoko na minada.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.