Mwanza watathimini utekelezaji wa mradi wa MMMAM
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa Mwanza, Daniel Machunda.
Na Tonny Alphonce, Mwanza
katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda amewataka wazazi na walezi kuwa makini katika malezi kwani ujio wa teknolojia umechangia kuwaharibu watoto wengi katika miaka ya hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kupitia utekelezaji wa programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, Machunda aliwataka wazazi na walezi kutosahau kutumia utamaduni wa kitanzania katika kuwalea watoto wao.
"Malezi asili ya kiafrika ni mazuri kwasababu yanazingatia maadili hivyo niwaombe wazazi wenzangu tuzingatie utamaduni wetu katika malezi ya watoto wetu" alisema Machunda.
Kwa upande wake meneja mradi, Christopher Peter kutoka TECDEN aliwataka watekelezaji wa programu ya MMMAM wazingatie malengo muhimu matano ambayo yanaubeba mpango huu wa MMMAM.
"Leo tumejipima hapa lakini katika maeneo haya matano bado hatujayatekeleza vizuri, kuna wengine mmefanya vizuri kwenye afya lakini kwenye lishe mmefeli, wengine mmefanya vizuri kwenye elimu lakini kwenye malezi yenye mwitikio mmefeli, wengine mmefanya vizuri kwenye ulinzi lakini kwenye usalama wa moto mmefeli" alisema Peter.
Peter aliwataka watekelezaji wa program hiyo kuhakikisha maeneo yote matano yanatekelezwa kwa usawa ili kusaidia mtoto kukua katika utimilifu wake.
Kikao hicho cha tathimini ya utekelezaji wa MMMAM kwa Mkoa wa Mwanza kimehudhuriwa na maafisa ustawi wa jamii, maafisa maendeleo ya jamii, maafisa elimu, maafisa mipango kutoka katika halmashauri za Ilemela, Nyamagana, Magu, Kwimba, Misungwi, Sengerema, Ukerewe na Buchosa.
Afisa Mradi, Christopher Peter.
Washiriki.
Washiriki.
No comments: