LIVE STREAM ADS

Header Ads

Taasisi, Kaya Rukwa zaagizwa kufanya kweli zisibaki nyuma

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katika muendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Mtu ni Afya iliyozinduliwa rasmi tarehe Mei 9 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Makongoro Nyerere ameendelea kusisitiza kaya na taasisi zote za mkoa wa Rukwa kufanya kweli kwa kuzingatia masuala ya usafi na afya ili zisibaki nyuma.

Makongoro ametoa ombi hilo ofisini kwake wakati wa mahojiano malumu na timu ya kampeni ya Mtu Ni Afya, Fanya Kweli Usibaki Nyuma.

‘’Kwa kutambua, umuhimu wa Afya, nakubaliana na kampeni ya Mtu Ni Afya,Fanya Kweli Usibaki Nyuma natoa maagizo tisa kuhusiana na Afya na ifikapo Oktoba 22 mwaka huu yawe yametekelezwa’’ amesema.
Amesema agizo la kwanza, ni kila kaya na taasisi zote za mkoa wa Rukwa kuwa na choo bora na choo hicho kiwe kinatumika.

‘’Agizo la pili, kila kaya na taasisi iwe na kifaa cha kunawia mikono na kuzingatia kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni katika nyakati malumu’’ amesema.

Katika agizo la nne, Nyerere ameagiza kila taasisi na kaya kufanya usafi wa maeneo ya makazi yao. Amesema agizo la tano ni kila mwananchi wa Rukwa awe anafanya mazoezi ya mwili kila siku kwa dakika 30.

Ombi la sita, Nyerere ameagiza kila kaya kuzingatia masuala ya hedhi salama pamoja na ombi la saba ni kaya zote ziwe zinazingatia lishe bora.

‘’Ombi langu la nane ni Kaya zote ziwe na utaratibu wa uaandaji wa maji safi na salama ya kunywa na ombi la tisa kila kaya izingatie matumizi sahihi ya nishati safi’’ amesema.
Katika hatua nyingine, Nyerere ameagiza kupewa taarifa ya kila wiki juu ya utekelezaji wa agizo hilo.

Naye Ofisa wa Afya mkoa wa Rukwa, Martin Emmanuel amesema mkoa wa Rukwa unatekeleza kampeni ya Mtu Ni Afya na kwa sasa wanasimamia ujenzi na matumizi ya vyoo bora.

‘’Mpaka sasa mkoa wa Rukwa tuna asilimia 83 ya kaya zenye vyoo bora na bado tunaendelea na zoezi hili la ujenzi na usimamizi wa vyoo bora ili kuepuka wananchi kupata magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu’’ amesema.

No comments:

Powered by Blogger.