LIVE STREAM ADS

Header Ads

Uzalishaji wa umeme wa gesi kuanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwonekano wa kisima cha gesi asilia Ntorya-2 kilichopo katika Kata ya Nanguruwe mkoani Mtwara.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na kampuni ya mafuta ya ARA lipo mbioni kuanza uzalishaji wa gesi asilia katika visima vya gesi vya Ntorya 1 na Ntorya 2 vilivyopo mkoani Mtwara.
***


Katika kuelekea hatua ya kuvuna gesi hiyo TPDC imejikita kwenye kutoa elimu ya mradi kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuelimisha viongozi wa serikali kwa ngazi zote za mkoa na wilaya pamoja na kufanya mikutano ya hadhara na wananchi watakao guswa na mradi huo. Kwa kuwa zoezi la uendelezaji linahitaji ardhi kwa ajili ya ujenzi wa mitambo na miundombinu mingine TPDC/ARA wanashirikiana na kampuni mshauri mwelekezi kwenye masuala ya uthamini APY-KEGS ili kuhakikisha masuala yote ya utwaaji wa ardhi yanafanyika kwa ustadi.

Akiongea katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Julai 06, 2024 katika kijiji cha Nanguruwe Meneja mradi wa Ntorya Patrick Kabwe alisema kuwa:-

"Shughuli za uzalishaji kwa visima hivi viwili vya gesi zinatarajiwa kuanza mwezi Aprili, 2025 ambapo kila kisima kitakuwa na auwezo wa kuzalisha futi za ujazo milioni 20 kwa siku , pia tunategema kuchimba kisima cha tatu kinachoitwa Chikumbi-1 ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha futi za ujazo milioni 20. 

Kwa awamu ya kwanza kwa visima vyote vitatu kutakuwa na uzalishaji wa jumla ya futi za ujazo milioni 60 kwa siku.

"Aidha awamu ya pili ya uzalishaji TPDC itachimba visima vinne katika kata ya Nanguruwe ambapo uzalishaji utafikia futi za ujazo milioni 140 kwa siku" alisema Kabwe.
Meneja mradi wa gesi Ntorya, Patrick Kabwe akielezea manufaa ya mradi huo.

Katika hatua nyingine Kabwe alishukuru uongozi wa Mkoa na Wilaya kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha mradi huu.

"Sisi TPDC pamoja na ARA Petroleum tunashukuru serikali ya Mkoa na Wilaya kwa ushirikiano wanaotupatia kwani bila wao tusingekuwa tumefika hapa, ushirikiano wanaotupatia ndio unasaidia mpaka sasa mradi unaendelea" aliongeza.


Naye Mwakilishi wa kampuni ya ARA Judith Kalugasha alisema "mradi huu wa gesi sio wa kwanza kwa Kata ya Nanguruwe, kinachoifanyika hapa hususani kwenye uthamini wa ardhi ni mwendelezo tu wa miradi mingine iliyopoita hivyo tunategemea ushirikiano kutoka kwa wanachi ili mradi huu ukamilike kwa wakati.
Mwakilishi wa kampuni ya ARA, Judith Kalugasha akizingumza kwenye mkutano wa hadhara eneo la Nanguruwe.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa TPDC, Oscar Mwakasege alieleza umuhimu wa miradi ya gesi asilia kwa jamii ikiwa ni pamoja na ajira, uboreshwaji wa huduma mbalimbali za kijamii kama afya, elimu , maji na utawala bora.

"TPDC tunafanya kazi na jamii hivyo tunawajibika katika kuleta ustawi wa huduma za kijamii kwenye vijiji ambavyo tunatekeleza miradi ya gesi asilia ikiwemo kijiji cha Nanguruwe" alisema.

Vilevile, Diwani wa Kata ya Nanguruwe, Patrick Simwinga alipongeza TPDC na Kampuni ya ARA Petroleum kwa kuwa na mpango mzuri wa kushirikisha jamii katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutekeleza mradi huo.

No comments:

Powered by Blogger.