UWADOMAMI wapata msafirishaji wilayani Misungwi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Umoja wa wafanyabiashara wadogo katika masoko na minada mkoani Mwanza (UWADOMAMI), umesaini makubaliano na kampuni ya malori ya Pamba Nyepesi kwa ajili ya kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara katika minada wilayani Misungwi
Makubaliano hayo yalisainiwa Julai 19, 2024 wilayani Misungwi ikiwa ni mwendelezo wa umoja huo kusaini mikataba na makampuni ya usafirishaji ili kuhakikisha mizigo ya wafanyabiashara inafika na kutoka salama katika minada.
Katibu wa UWADOMAMI Mkoa Mwanza, Davis Philipo alisema awali iliibuka changamoto kwa wasafirishaji mizigo minadani hatua iliyoilazimu UWADOMAMI kwa kushirikiana na Mwanasheria wake kuandaa mikataba ili kuondoa changamoto hizo.
Alisema baadhi ya changamoto ilikuwa baadhi ya wasafirishaji kutowajibika wanapopoteza mizigo ya wafanyabiashara kwa kuwa hakukuwa na makubaliano yoyote huku wengine wakienda mbali zaidi na kutowaheshimu viongozi wa UWADOMAMI wakati wanabeba mizigo ya wanachama wake.
"Tumeanza kusaini mikata mwaka huu 2024, hapo awali kila mtu alikuwa anajifanyia mambo anavyotaka, sasa hatuwezi kuwa na jamii isiyofuata utaratibu ama sheria ndiyo maana tumeingia makubaliano na wasafirishaji wote minadani ili tufanye kazi kwa kuheshimiana" alisema Philipo.
Hata hivyo mikataba hiyo imepokelewa vyema na wasafirishaji ambao walisema itasaidia kuondoa wakorofi wachache ambao walikuwa wanafanyaka kazi kwa mazoea na kuwaharibia wengine wanaoheshimu kazi hiyo.
Tayari UWADOMAMI imeingia makubaliano ya miaka mitatu na wasafirishaji mizigo kwenye minada katika wilaya za Nyamagana, Ilemela, Kwimba, Misungwi pamoja na Magu na Sengerema kwa baadhi ya minada hivyo mchakato wa kukamilisha minada yote bado unaendelea katika wilaya hizo.
Katibu wa UWADOMAMI Mkoa Mwanza, Davis Philipo (kulia) na Meneja wa kampuni ya malori ya Pamba Nyepesi, Masanja Paul (kushoto) wakisaini mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kufanya kazi pamoja katika masoko na minada wilayani Misungwi.
Wanaoshuhudia ni viongozi wa UWADOMAMI wilayani Misungwi ambapo kulia ni Mwenyekiti na kushoto ni Katibu Msaidizi.
Katibu wa UWADOMAMI Mkoa Mwanza, David Philipo (kulia) akimkabidhi mkataba Meneja wa Kampuni ya Pamba Nyepesi, Masanja Paul (kushoto) baada ya umoja huo kuingia makubaliano na kampuni hiyo kwa ajili ya kusafirisha mizigo ya wafanyanyiashara katika masoko na minada wilayani Misungwi.
Wanaoshuhudia ni viongozi wa UWADOMAMI wilayani Misungwi wakiongozwa Mwenyekiti (wa pili kulia), Makamu Mwenyekiti (wa tatu kulia) na Katibu Msaidizi (wa nne kulia).
PIA>>> BONYEZA HAPA KUSOMA ZAIDI
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
No comments: