Wakatoliki waaswa kuwatunza Mapadri
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waamini wa Kanisa Katoliki wameaswa kuwalea na kuwatunza mapadri kwa kuwa mapdri hao wametoa maisha yao kwa Mungu ili kuwasaidia watu kuishi maisha ya utimilifu wa kiroho kwa kuwaongoza kupitia maandiko na kufikia ufalme wa Mbingu.
Rai hiyo imetolewa Agosti 22, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alipokuwa akiongea na waamini wa Jimbo la Mbulu wakati wa Jubilei ya Miaka 25 ya Upadri wa Mhashamu Baba Askofu Antony Lagwen iliyofanyika jimboni humo.
Alisema kuwa kila muamini kwa nafasi yake anatakaiwa kujitafakari kama anatimiza wajibu wake sawa sawa kwa Mungu ikiwa ni pamoja na kujitolea kuwalea hao wanaowaita ‘Baba’ kwa kuwa wamekwisha jitoa sadaka kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu.
“Waamini wenzangu, tunatakiwa kuwalea hawa tunaowaita ‘Baba’ ‘Baba’ ambao ni maaskofu na mapadri, hao ni binadamu na wanamahitaji muhimu kama sisi mathalani chakula, nguo, matibabu, usafiri na nyumba za kuishi, hivyo nguvu tunazoweka katika ujenzi wa makanisa ni sawa, kutoa sadaka ni sawa, kutoa zaka ni sawa. Kwa umoja huo huo tushiriki kutimiza mahitaji yao ya kimwili ili hata ya kiroho yaweze kwenda vyema” alisisitiza Simbachawene.
Aidha aliongeza kuwa ni wajibu wa waamini kutambua kuwa wazazi wa mapadri hawa walitoa watoto wao sadaka kwa Mungu na hivyo ni wajibu wa kanisa ambao ni waamini wote kushirikiana katika kuwalea na kuwatunza kwa hali na mali.
Simbachawene amemuomba Mhashamu Askofu Antony G. Lagwen kupokea salaam za pongezi kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuahidi kuendelea kushirikiana na kanisa Katoliki katika Nyanja mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Awali Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu katika Mahubiri yake aliwasisitiza mapadri kutokuwazuia waamini kufanyia Jubilee kwa kuwa Upadri ni zawadi ya Mungu katika nafasi zao.
“Tunatakiwa kuwa kitu kimoja na Mungu na Mungu anakuwa kitu kimoja na sisi, hivyo tuukanyage kabisa uovu na tuushinde uovu kwa wema” aliongeza Mhashamu Lebulu.
Vilevile, katika Salaam za shukrani Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu Mhashamu Antony Gaspar Lagwen ambaye ameadhimisha Jubilee ya miaka 25 (1999-2024) ya Upadri, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na Kanisa na kuhakikisha kunakuwa na maendeleo kwa wananchi.
Mhashamu Lagwen aliomba Serikali kuendelea kuwa karibu na Kanisa Katoliki sio tu kwa maendeleo ya Kanisa bali ili jamii ipate huduma na kujijenga inavyopasa katika masuala ya uboreshaji wa mazingira, utawala bora na kulinda utu wa mtu wakati wote kwa ustawi wa taifa.
No comments: