MAJALIWA atoa maagizo mapambano dhidi ya utapiamlo, udumavu
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka mawaziri wa kisekta, wakuu wa mikoa, wilaya, halmashauri na taasisi mbalimbali kuupa kipaumbele na kushiriki kwenye mkutano mkuu wa wadau wa lishe nchini ili kupata ushauri, maoni na mapendezo ya namna bora ya kukabiliana na changamoto za lishe zinazosababisha utapiamlo na udumavu hasa kwa watoto chini ya miaka mitano.
Majaliwa alitoa wito huo Oktoba 03, 2024 jijini Mwanza wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 10 wa wadau wa lishe nchini ukiwa na kaulimbiu ya "kuchagiza mchango wa wadau wa kisekta ili kudumisha matokeo bora ya hali ya lishe nchini Tanzania".
"Idadi ya wadau na wizara za kisekta zinatakiwa ziongezeke zihudhurie mkutano huu. Tamisemi, kilimo, afya, maendeleo ya jamii, mifugo na uvuvi zilete mawaziri waudhurie mkutano huu wapate maoni ya wadau na kufanya tathmini kuhusu utekelezaji wa afua za lishe, lazima wawepo kila mmoja apate jukumu lake, pia maafisa maendeleo wa halmashauri na maafisa lishe ili kushirikiana na wakuu wa wilaya na mikoa kutekeleza afua za lishe na mipango ya Serikali" alisema Majaliwa.
Majaliwa alisema takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa mwaka 2022 zinaonyesha theluthi moja ya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 wamedumaa, huku akiwataka wadau hao kutumia fursa ya mkutano huo kubadilishana uzoefu na mbinu zinazotumika katika utekelezaji wa programu za lishe nchini, ikiwa ni pamoja na ubunifu katika kukabiliana na changamoto za lishe.
"Ni dhahiri kuwa kila mmoja wetu anatambua kuwa lishe huathiriwa na mambo mbalimbali zaidi ya sekta ya afya. Hivyo, kwa kuhusisha wadau wa sekta kama vile kilimo, elimu, maji na usafi wa mazingira, na ulinzi wa kijamii, inawezesha kuweka mikakati endelevu ya kuboresha matokeo ya chanya ya lishe bora. Sababu kuu za kutilia mkazo ushiriki wa wadau wa kisekta wa lishe nchini Tanzania ni pamoja na kushughulikia sababu za msingi za utapiamlo kama vile umaskini, uhaba wa chakula, na mazoea duni ya utunzaji vyakula, pia kuboresha utumiaji wa rasilimali, kuunda ushirikiano na kujenga msingi madhubuti wa lishe" alisema.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda aliiomba Serikali kufikiria upya mpango wake wa kuipunguzia majukumu Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kwani imekuwa nguzo muhimu katika elimu na tafiti za lishe nchini, huku akishauri kushirikishwa kwa viongozi wa kimila na wa dini katika utoaji wa elimu ya lishe kwenye jamii kwani wana nguvu na ushawishi na itasaidia kuongeza uelewa na mapambano dhidi ya utapiamlo kufanikiwa.
"Nashukuru ninanapoona serikali inalivalia njuga suala hili kwa sababu wakati mwingine ni aibu na linatushushia hadhi kwa sababu ni jambo ambalo liko ndani ya uwezo wetu, naamini taratibu tutalichukulia kwa uzito mkubwa na kupunguza tatizo hili" alisema Pinda.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi alisema Serikali imeendelea kuhakikisha sekta zinazohusika na utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa masuala ya Lishe zinaingiza masuala hayo katika mipango na bajeti kila mwaka huku ofisi ya Waziri Mkuu ikiendelea kuratibu ufuatiliaji na tathmini pamoja na kuhakikisha wanawakutanisha mara kwa mara wadau kujadili utekelezaji wa afua za lishe nchini.
"Kwa takwimu tulizonazo sasa za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (2022) zinaonesha viwango vya udumavu na uzito mdogo (underweight) kwa watoto chini ya miaka mitano vimekuwa vikipungua. Katika kipindi cha mwaka 2018 na 2022 udumavu ulipungua kutoka asilimia 32 iliyokuwa mwaka 2018 hadi asilimia 30 kwa mwaka 2022, na uzito mdogo ulipungua kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 katika kipindi hicho. Jitihada za kukabiliana na changamoto hizi zimekuwa zikifanyika katika ngazi ya taifa na mkoa husika" alisema Lukuvi.
Meneja mradi wa kuhamasisha afua za Lishe kwa akina mama na watoto kwa kuangalia usawa wa kijinsia (Grow Enrich Project) kutoka World Vision Tanzania, Shukrani Dickson alisema ili kusaidia Serikali kukabiliana na changamoto hiyo, shirika hilo linafundisha akina mama ngazi ya jamii namna ya kuandaa mlo kamili kwa ajili ya watoto, kuhahakikisha kila mwaka watoto wanapata chanjo ya Vitamini A na kuwawezesha wahudumu wa afya kutembelea kaya kwa kaya ili kuwafundisha akina mama namna ya kuwatunza watoto na kuhudhuria kliniki na kupima watoto uzito.
"Tunao mpango mkubwa sana kama World Vision Tanzania kuhamasisha ulimaji wa viazi lishe, hivi viazi lishe na maharage lishe vinaongeza virutubisho vikubwa sana kwa watoto tunawahimiza wanajamii kulima viazi lishe kwa kuwapatia mbegu na utaalamu mbalimbali ili kuhakikisha kwamba watoto wanapata vyakula ambavyo vinaongeza virutubisho vinavyopatikana kwenye maeneo yao" alisema Shukrani.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba alisema "katika mkoa wetu wa Mwanza hali ya udumavu kwa sasa ni asilimia 28 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022 ukilinganisha na asilimia 39 mwaka 2018. Kwenye uzito pungufu tuna asilimia 2.8 lengo la kitaifa ni asilimia tano lakini ukondefu ni asilimia 1.8 na lengo la kitaifa ni asilimia tatu nayo ukiangalia bado tunafanya vizuri".
Mkutano huo uliafikiana maazimio matano ambayo ni masuala ya huduma za lishe yajumuishwe katika dira ya taifa 2050 na kuimarisha huduma za lishe kwenye ngazi ya jamii ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hii, kuimarisha uratibu na utekelezaji wa vipaumbele vya Mpango wa Pili Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (Nutrition Multisecterial National Action Plan II - NMNAP II) kwa kuhakikisha kila Wizara za kisekta na wadau wa maendeleo wanawajibika kutekeleza afua za lishe kulingana na Mpango, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza afua za lishe, na kuimarisha upatikanaji na matumizi ya taarifa za lishe katika ngazi zote.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA>>> Bonyeza hapa kusoma zaidi
No comments: