TANESCO Mwanza wawatembelea wateja kuadhimisha 'Wiki ya Huduma kwa Wateja 2024'
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa Mwanza, wameendelea na maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja kwa kuwatembelea wateja ili kupata mrejesho wa huduma wanayoipata.
Zoezi hilo la kuwatembelea wateja limefanyika Jumanne Oktoba 08,2024 likiongozwa na Meneja wa TANESCO Mkoa Mwanza, Mhandisi Godlove Mathayo.
Akiwa mtaa wa Ibanda Kazamoyo Kata ya Kirumba wilayani Ilemela, Mhandisi Mathayo alisema mtaa huo ulikuwa na changamoto ya kupata umeme mdogo na hivyo kuleta adha kwa wateja ambapo baada ya shirika kupokea malalamiko ya wateja, lilishughulikia changamoto hiyo kwa kufunga transifoma yenye uwezo mkubwa.
"Baada ya kupokea malalamiko ya wateja, mafundi wetu walifika na kukagua changamoto iliyokuwepo kwenye mtaa huu na kubaini kuna 'low voltage' na tukaanzisha mradi wa matengenezo uligharimu shilingi milioni 35 na sasa changamoto tumeitatia kabisa" alisema Mhandisi Mathayo.
Mmoja wa wakazi wa mtaa huo, Thomas Biashara alisema walikuwa na changamoto ya kupata umeme wa kutosha kiasi cha kushindwa kuwasha taa hasa nyakati ambapo baada ya kutoa taarifa TANESCO ilishughulikiwa kwa wakati na hivyo kwa namna wanavyopokea malalamiko ya wateja na kuyafanyia kazi kwa wakati.
Changamoto nyingine kama hiyo ilijitokeza katika Mtaa wa Nyambiti Kata ya Buzuruga ambapo pia TANESCO baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wateja walifika na kuitatua kwa kutenganisha njia ya umeme kwenye mashine za nafaka zilizokuwa kwenye mtaa huo.
"Kwa sasa hakuna changamoto kabisa, tunaweza kuwasha mashine hata mbili kwa wakati mmoja. Tunawaahukuru TANESCO kwa kututembelea" alisema Khamis Daud, mfanyabiashara wa nafaka Nyambiti.
Pia Mhandisi Mathayo na timu yake ya wafanyakazi walifika katika Mtaa wa Igudija Kata ya Kisesa na kukagua mradi mpya wa usambazaji umeme ambao umefikia hatua ya kusimika nguzo na kueleza kuwa wiki chache zijazo wakati wa mtaa huo watapata nishati ya umeme.
"Tumefarijika kupata mradi huu wa umeme, utaondoa changamoto ya uandaaji wa vipindi vya masomo na uchapishaji mitihani. Pia hapa tuna wanafunzi wa bweni, tunakwenda kuondokana na changamoto ya giza" alisema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Witzon iliyopo Mtaa wa Igudija.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Igudija B, Fomu Lushinge alisema ujio wa umeme katika Mtaa huo ambao ni maarufu kama majengo mapya utachochea shughuli za maendeleo/ kiuchumi kwa wakazi wake kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo uchimeleaji na mabanda ya kuonyesha mpira kwani huduma hizo wamekuwa wakizifuata mbali.
Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja hufanyika kila mwaka katika wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba ambapo kwa mwaka huu ni kuanzia Oktoba 07-11, 2024.
Na George Binagi GB Pazzo, BMG
Meneja wa TANESCO Mkoa Mwanza, Mhandisi Godlove Mathayo (wa nne kushoto) akiwa na wafanyakazi wa shirika hilo walipomtembelea mteja (wa tano kushoto) katika Mtaa wa Ibanda Kazamoyo.
Meneja wa TANESCO Mkoa Mwanza, Mhandisi Godlove Mathayo (wa tano) akiwa na wafanyakazi wa shirika hilo walipomtembelea mteja (wa nne kulia) katika Mtaa wa Nyambiti.
Meneja wa TANESCO Mkoa Mwanza, Mhandisi Godlove Mathayo (watano kushoto) akiwa na wafanyakazi wa shirika hilo na Mwenyekiti Mtaa wa Igudija B (wa tano kulia) na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Wizon (wa nne kishoto).
Kazi ya kusimika nguzo ikiendelea katika Mtaa wa Igudija Kata ya Kisesa.
PIA>>> Bonyeza hapa kusoma zaidi
No comments: