LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Kikwete atoa mwelekeo wa Wiki ya Vijana kitaifa jijini Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ametaja shughuli nne zinazofanyika katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa mkoani Mwanza ikiwemo kongamano la fursa na kuwajengea uelewa wa masuala mbalimbali vijana.

Akizungumza Oktoba 09,2024 na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu maadhimisho hayo ambayo yameanza Oktoba 08, 2024, Ridhiwani alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua wiki hiyo katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza Oktoba 11, 2024.

Waziri Ridhiwani alitaja shughuli zitakazofanyika kwenye wiki hiyo kuwa ni pamoja naKongamano la kuwajengea uelewa wa fursa za ujasiriamali, ubunifu wa kidijitali katika kujifunza na kujiajiri sambamba na elimu ya Sera mpya ya maendeleo ya vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024.

Pia alisema kutakuwa na maandamano ya amani ya vijana na watashiriki 1000 wakiwa wamebeba jumbe mbalimbali ambazo serikali itazifanyia kazi.

“Kutakuwa na Maonesho ambayo hutoa fursa kwa vijana kuonesha bunifu zao na kwa wadau wa maendeleo ya vijana kutoa huduma, elimu na taarifa kwa jamii hususan zile zinazoendana na malengo ya Taasisi zao na zenye lengo la kuleta mabadiliko chanya na kuhamasisha ustawi na maendeleo ya vijana nchini”alisema.

Alifafanua malengo ya wiki hiyo kuwa ni kuwakutanisha vijana kujadili furs ana changamoto zinazowakabili, kuhamasisha kushiriki katika program mbalimbali za usaidizi wa jamii kwa njia ya kujitolea, kuwawezesha vijana kupata uzoefu wa namna ya utekelezaji wa masuala ya kiuchumi na kijamii.

“Pia wiki hii inalenga kuwahamasisha vijana watambue kuwa wao ni sehemu ya jamii na wenye jukumu katika kushughulikia changamoto za kijamii kama vile VVU na UKIMWI, Ukiukwaji wa haki za binadamu na watoto, kushiriki katika majukumu ya kiraia ikiwamo kupiga kura na kushiriki vikao vya maendeleo katika jamii”alisema.

Kuhusu kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Ridhiwani alisema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhitimisha sambamba na Kumbukumbu ya Miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere itakayofanyika Kanisa Katoliki la Nyakahoja mkoani Mwanza.

Alitoa wito kwa wananchi na vijana kujitokeza kushiriki katika maadhimisho ya wiki hiyo ya vijana inayofanyika uwanja vya Furahisha kuanzia Oktoba 8-13, 2024 na Kilele cha Mbio za Mwenge kitakachofanyika Uwanja wa CCM Kirumba Oktoba 14, 2024.

No comments:

Powered by Blogger.