BITEKO: Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba katika kuboresha huduma kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Ambapo katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali imenunua mashine za altrasound 457 na hivyo kufikisha idadi ya mashine 970 ambazo zimesambazwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Taifa, Hospitali maalum, Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati.
Dkt. Biteko aliyasema hayo Oktoba 09, 2024 jijini Arusha wakati akifungua Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa Chama cha Wana Radiolojia Tanzania (TARA), lenye kaulimbiu inayosema Tafasiri ya majibu ya vipimo na maadili (Pattern Recognition and Ethics)”.
Akifafanua zaidi kuhusu uwekezaji uliofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka mitatu, Dkt. Biteko alisema “Serikali imeweza kununua mashine za kidigitali za x-ray 386 hivyo kufikia jumla ya mashine 469, kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa, Hospitali ya Maalum, Hospitali ya Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya na Vituo vya Afya”.
Aidha Serikali imeendelea kuboresha huduma katika Hospitali ya Taifa, Hospitali Maalumu na Hospitali za Kanda na kufikisha jumla ya mashine saba za MRI zilizonunuliwa na kufikia mashine 13 katika hospitali za umma sambamba na kusambazwa kwa mashine za CT scan katika mikoa yote.
“Kama Rais asingefanya uwekezaji huu mkubwa ni fedha kiasi gani zingeenda kutumika nje ya nchi, lakini vifaa pekee haviwezi kutoa majibu isipokuwa nyinyi wataalamu, kwa niaba ya Serikali tunawashukuru sana na tunatambua mchango wenu” alisema Dkt. Biteko.
Aliongeza kuwa Serikaki si tu inataka kuimarisha sekta ya miundombinu na maji bali pia kuboresha afya za Watanzania na kuwa kwa sasa nchini imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.
Aidha Dkt. Biteko aliwataka wanaradiografia kufanya kazi kwa weledi, kuiheshimu taaluma yao kuilinda na kuionea wivu kwa kuwa Serikali licha kuwekeza katika vifaa inaona umuhimu wao na ndio maana imeendelea kuwasomesha wataalamu hao.
“Hakuna mtu atakayekupa heshima yako bila wewe kuiheshimu, furukuteni ili mtu aone umuhimu wenu, furukuteni hakuna sababu ya kulalamika nendeni mkawahudumie watu kwa upendo ili kweli waone Serikali yao ipo kwa ajili ya kuwahudumia na ilindeni taaluma yenu kwa wivu mkubwa” alisisitiza Dkt. Biteko.
Vilevile, alielekeza taasisi za TMDA, NHIF na TBS nazo zipate wa radiografia katika ofisi hizo ili kuleta ufanisi wa kazi katika maeneo yanayohusu huduma za radiolojia. Sambamba na kuitaka Wizara ya afya kufanyiakazi changamoto zote wanazokabiliana nazo wanaradiografia nchini.
Akimalizia hotuba yake, Dkt. Biteko aliwasihi washiriki wa Kongamano hilo kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuchagua viongozi watakaosaidia kuchochea maendeleo katika jamii.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa Rais Dkt. Samia amefanya mapinduzi katika sekta ya afya katika muda mfupi ikiwa ni pamoja kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi kutoka 400 hadi 100.
“Katika kuboresha huduma za kibingwa katika taasisi na Hospitali ya taifa, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imepata mashine ya PET-CT ambayo hufanya uchunguza wa awali wa saratani na mgonjwa kupata matibabu mapema” alisema Dkt. Mollel.
Aliongeza pamoja na huduma za kibingwa na mashine za kisasa kutibu kwa kutumia tundu dogo sasa zinapatikana Taasisi ya mifupa na mishipa ya fahamu (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete (JKCI) na Hospitali ya Benjamini Mkapa”.
Dkt. Mollel alifafanua kuwa watoto wenye vibiongo wana uwezo wa kunyooshwa mgongo kupitia vifaa vilivyonunuliwa na Serikali na wagonjwa wa uvimbe wa chini ya sakafu ya ubongo, pia Serikali imenunua vifaa vinavyoweza kutibu ugonjwa huo bila kufungua ubongo.
“Tanzania ni nchi ya nne Afrika kumiliki PET SCAN ya kumgundua mtu mwenye aina yoyote ya kansa na kutibu ndani ya nchi bila kwenda nje, pia nchi yetu ina kiwanda cha kuzalisha mionzi tiba na kabla ya hapo ilikuwa inanunuliwa kwa gharama kubwa nchini Afrika Kusini au Uturuki, hivyo tumepunguza rufaa za nje ya nchi kwa asilimia 97” alisema Dkt. Mollel.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alisema katika Mkoa huo Serikali imetoa shilingi bilioni 72 katika sekta ya afya ambapo shilingi bilioni 32 imetumika kwa ajili ya kununua vifaa tiba na dawa, aidha fedha nyingine zimetumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali katika ngazi mbalimbali.
“Ninamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia wewe kwa kazi kubwa nzuri aliyofanya katika sekta ya umeme ikiwemo uendelezaji wa mradi wa Bwawa la Julius Nyerere na hadi mradi huo kukamilika na kuanza kutoa umeme ambao unachagiza ukuaji wa uchumi. Arusha tumezindua mradi wa REA tutaenda kukamilisha kupeleka umeme katika vitongoji 1025 tunakushuru sana kwa usimamizi wako katika miradi hii” alisema Makonda.
Rais wa Chama cha Wanaradiografia Tanzania (TARA), Bakari Msongamwanja alisema kuwa TARA iliundwa mwaka 1976 kwa lengo la kuwakutanisha wataalamu wa radiografia pamoja na kuboresha taaluma hiyo nchini na kimataifa.
Msongamwanja alibainisha kuwa TARA imekuwa na uhusiano mzuri na vyama vya kitaaluma Afrika na duniani na hivyo imeweza kushika nafasi mbalimbali ikiwemo kuongoza dawati la elimu Kanda ya Afrika.
Aliongeza kuwa TARA imeshiriki katika kazi mbalimbali za kukuza taaluma ya radiologia nchini ikiwemo kuandaa kanuni za mpango wa elimu endelevu.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutenga fungu na kusaidia wanaradiografia kujiendeleza tutajitahidi kuhakikisha wataalamu wanafanyakazi kwa weledi na kuzingatia maadili” alisema Bakari.
No comments: