Silinde afungua maadhimisho ya Ushirika wa Akiba na Mikopo 2024
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amewataka viongozi wa vyama vya ushirika nchini (AMCOS), kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA na kuacha kufanya kazi kwa kutumia mifumo ya zamani ili kutoa huduma bora katika vyama hivyo.
Silinde ameyasema hayo Jumatatu Oktoba 21, 2024 wakati akifungua maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ushirika wa akiba na mikopo duniani yanayofanyika kitaifa uwanja wa Mirongo jijini Mwanza.
Pia Silinde alisema ili kuweza kuleta maendeleo katika vyama vya ushirika viongozi wa vyama hivyo wanatakiwa kufanyakazi kwa kufuata sheria na miongozo.
"Viongozi waendelee kusimamia ushirika kwa kufuata misingi, kanuni, sheria na miongozo kwa ajili ya kuleta maendeleo" alisema Silinde.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde.
Naye Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mwanza, Peter Kasele akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya aliwataka wananchi kutumia fursa ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ushirika wa akiba na mikopo katika kujipatia elimu ya masuala ya fedha.
Kasele alisema Serikali ya Mkoa inatambua umuhimu na mchango wa vyama vya ushirika katika kuleta maendeleo kwa watumishi pamoja na wananchi.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mwanza, Peter Kasele.
Kwa upande wae MwenyeKiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), Aziza Mshana alitoa shukuani kwa Serikali katika kuthamini mchango wa ushirika wa akiba na mikopo katika kukuza uchumi.
Maadhimisho hayo yanafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia Oktoba 20, 2024 hadi Oktoba 24, 2024 yakiwa na kaulimbiu isemayo "ulimwengu mmoja kupitia Uushirika wa kifedha" yakianyika kwa mara ya 76 duniani, kwa mara ya 15 nchini Tanzania.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu Cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), Aziza Mshana.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
PIA>>> BONYEZA HAPA KUSOMA ZAIDI
No comments: