LIVE STREAM ADS

Header Ads

SCCULT yataka michango ya wanachama wa SACCOS kuwasilishwa kwa wakati

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT), Aziza Mshana amesema baadhi ya waajiri wanakwamisha utendaji kazi wa vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) kutokana na kuchelewesha michango ya wanachama wake.

Mshana ameyasema hayo Jumatatu Oktoba 21, 2024 wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ushirika wa akiba na mikopo duniani yanayoanyika kitaifa jijini Mwanza na kuongeza kuwa hali hiyo imekuwa kikwazo kwa SACCOS mbalimbali nchini kujiendesha.

Akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mshana alisema vyama vya ushirika vinapitia changamoto nyingi lakini hii ya kucheleweshwa kwa fedha hizo imekuwa na athari kubwa zaidi hasa ikizingatiwa kuwa SACCOS haziruhusiwi kukusanya amana kutoka kwa umma na hivyo kukosa vyanzo vingine vya kupata fedha za kuendesha shughuli zao.

"Fedha hizo hucheleweshwa kwa kipindi kirefu hadi miezi mitano, hii inaleta kadhia kwenye utoaji wa huduma, ukizingatia SACCOS zinatumia fedha za wanachama wake tu na haturuhusiwi kukusanya amana kutoka kwa umma" alisema Mshana.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde akifungua maadhimisho hayo licha ya kueleza kusikitishwa kwake na ucheleweshaji wa fedha hizo, amekemea kitendo hicho na kusema kuwa fedha hizo sio mali ya mwajiri bali ni mali ya mwajiriwa ambaye ni mwanachama wa SACCOS na malimbikizo hayo yamekuwa yakizikosesha ukwasi SACCOS na nguvu ya kuhudumia wanachama wake kwa wakati.

"Hili halikubaliki na naomba waajiri waliache mara moja, kanuni za huduma ndogo za fedha kanuni ya 88 imeelekeza SACCOS na waajiri kusaini makubaliano ambayo yatasaidia kuondoa changmoto hii, ofisi yangu itafanya mazunguzo na wahusika ikiwemo na wakurugenzi wa halmashauri" alisema Silinde.

Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC), Dkt. Benson Ndiege aliwaasa wana ushirika wa akiba na mikopo kuendelea kuwa wabunifu ili kuwa na utofauti katika kuwahudumia wanachama.

Mjumbe wa Bodi ya TRA SACCOS, Mbogo Kerenge alisema wanatoa elimu kwa wanachama wao ili wasiathirike na mikopo ya kausha damu ambayo imekuwa ikirudisha nyuma uchumi wa wananchi.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ushirika wa akiba na mikopo yanayofanyika jijini Mwanza.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT), Aziza Mshana akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Bara, Dkt.Benson Ndiege akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mrajis Msaidizi vyama vya kifedha Tanzania, Josephat Kisamalala (kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde wakati wa ufunguzi wa maadhimisho.
Baadhi ya wanachama wa vyama vya ushirika wa akiba na mikopo wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ushirika wa kifedha duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.