LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali yatoa bilioni 60 kuboresha bandari za Ziwa Victoria

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Watanzania tujiandae na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
***

Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inakamilisha maboresho ya kupokea meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu, lengo likiwa ni kuwarahisishia usafiri wananchi wa maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.

Meli hiyo ya abiria inayojengwa itakuwa kubwa zaidi Afrika Mashariki ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20, na magari makubwa matatu, hivyo kuongeza maradufu uwezo wa abiria ikilinganishwa na MV Victoria inayobeba abiria 600 kwa sasa.

Tayari serikali imewekeza kiasi cha Shilingi bilioni 60 kwa ajili ya kuboresha bandari tatu kuu za Ziwa Victoria.

Uwekezaji huu mkubwa katika bandari za Kemondo, Bukoba na Mwanza Kaskazini unatarajiwa kuboresha ufanisi na uwezo wa huduma za usafiri katika eneo hilo.

Kazi ya kuboresha Bandari ya Kemondo, imekamilika kwa asilimia 98 na hatua za mwisho zinahusisha kusafisha eneo kabla ya kuzinduliwa rasmi na mradi wa kuboresha Bandari ya Bukoba kwa sasa umefikia asilimia 75.

Maboresho yanayoendelea yanakusudia kuongeza kina cha maji kutoka mita 3.5 hadi mita 5 katika Bandari za Kemondo na Bukoba.

Aidha mabadiliko mengine yanahusisha kuongeza urefu wa gati kutoka mita 75 hadi 92, kuboresha eneo la sakafu kwa kuimarisha muundo wa zege, na kufunga uzio wa kuimarisha usalama huku maboresho mengine yakijumuisha ujenzi wa maeneo ya kusubiri abiria, vituo vya ukaguzi wa mizigo, mfumo wa umeme wa kisasa, na kinga ya upepo.

Aidha serikali inaanzisha vituo vya huduma vya sehemu moja katika bandari zote zinazoboreshwa, ikijumuisha huduma za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Misitu, Uhamiaji, Afya, na Wakala wa Forodha na Uondoshaji Mizigo pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama ili kuboresha utoaji wa huduma.
#KaziInaendelea

No comments:

Powered by Blogger.