Zaidi ya Bilioni 18 zakarabati miundombinu ya mabasi yaendayo kasi Dar
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Mradi huo wa awamu ya kwanza, upo chini ya Mradi wa OPBRC (Output and Performance-Based Road Contract) uliosainiwa rasmi Septemba 07, 2018.
Kufanikiwa kwa mradi huo wa matengenezo ya miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) ni jitihada zinazofanywa na Rais wa awamu ya sita, Dkt.Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha adha ya usafiri inaondoka katika Jiji la Dar es Salaam.
Mradi huo wa muda mrefu, ulianza rasmi Aprili 01, 2019 ukitekelezwa na Mkandarasi M/s Bharya Engineering & Contracting Co. Ltd (BECCO) kwa utekelezaji wa muda wa miezi sitini (60) yaani miaka mitano.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi John Mkumbo ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 18.509 ambazo zinajumuisha makundi matatu ya kazi.
Ameyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na mradi wa matengenezo ya miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 21.4 ikihusisha, Barabara ya Morogoro kuanzia Ferry mpaka Kimara Mwisho, Barabara ya Kawawa (Magomeni Mapipa – Morocco), na Barabara ya Msimbazi (Fire – Msimbazi BRT Station).
Mhandisi Mkumbo amesema TANROADS pia inatekeleza kazi za maboresho ya sehemu zilizoharibika ikihusisha matengenezo makubwa ya tabaka la lami katika sehemu zilizoharibika.
TANROADS imesema imefanya kazi za dharura zikihusisha matengenezo ya uharibifu ambao haukutarajiwa kama kazi ya kuondoa tope, mchanga na takataka kwenye daraja na eneo la barabara wakati wa mafuriko na mvua kubwa, na matengenezo ya miundombinu yatokanayo na ajali za barabarani kwenye miundombinu ya BRT awamu ya kwanza.
#KaziInaongea
No comments: