LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kaya laki saba kufikiwa na nishati safi ya kupikia

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mama, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumwondoa Mtanzania kwenye adha na maradhi yanayotokana na nishati chafu ya kupikia na katika kufanikisha hilo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2025 kaya 700,000 zitakuwa zimewezeshwa kutumia nishati safi ya kupikia mijini na vijijini kwa njia ya umeme.

Hatua hiyo inalenga kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya mishati safi ya kupikia (2024/2034) unaolenga kuwafikia asilimia 80 ya watanzania.

Kimsingi Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umejipanga kuwezesha Kaya hizo pamoja na kaya zipatazo milioni saba kutumia nishati safi.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amebainisha hayo hivi karibuni jijini Baku nchini Azerbaijan akizungumza katika mjadala wa Nishati Endelevu kwa Wote katika Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi maarufu kama COP29.

“Katika uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumezindua Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na lengo ni hadi kufikia mwaka 2034; asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi za kupikia,” amefafanua.

Amesema katika kufikia lengo hilo; REA imepewa jukumu la kutekeleza mkakati huo na kwamba tayari utekelezaji wake umeanza na kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 kaya zipatazo laki saba zitawezeshwa kutumia nishati safi ya kupikia.

“Tunatarajia kwa kipindi cha miaka 10 ya utekelezaji wa mkakati huu wa nishati safi ya kupikia tuwe tumezifikia kaya milioni saba, na tayari tumeanza na kwa mwaka huu tutazifikia kaya laki saba” amesema Mhandisi Saidy.

Hadi sasa Serikali imefanikiwa kufikisha umeme kwa takriban vijiji vyote na sasa imeanza kusambaza katika vitongoji na kwamba inaendelea kuhamasisha wananchi kutumia umeme kwa ajili ya kupikia hasa ikizingatiwa kuwa umeme unaotokana na nishati jadidifu ni nishati safi kwa 100% na hauna madhara kwa mazingira na kwa afya za mtumiaji.

Amesisitiza kuwa matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia hayatumii gharama kubwa ikilinganishwa na matumizi ya nishati zingine na pia yanaokoa muda ambao mwananchi angetumia kutafuta nishati zingine na muda pia wa kupika.
#KaziInaongea

No comments:

Powered by Blogger.