Serikali kupitia upya kanuni za uendeshaji maduka ya dawa za binadamu
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kujali afya za wananchi wake, kwa kusimamia sekta ya afya, ambapo imeielekeza Wizara ya Afya kupitia upya kanuni zinazohusu uendeshaji wa maduka ya dawa yaliyopo pembezoni mwa hospitali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amezungumza Disemba 04, 2024 jijini Dodoma wakati wa kufungua mkutano mkuu wa 54 wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST) na kueleza kuwa, hatua za kudhibiti matumizi holela ya dawa ni muhimu katika kulinda maisha ya wananchi na kujenga imani ya jamii kwa huduma za afya.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kuwepo utaratibu unaoruhusu uuzaji wa dawa katika maeneo hayo, huku hatua za kudhibiti wizi wa dawa na uvunjifu wa sheria zikizingatiwa na kuagiza waajiri wote wa Sekta ya Afya, kuhakikisha kuwa Wafamasia waliopo kazini, ambao ni wanachama wa PST, wanapewa ruhusa ya kushiriki mikutano ya chama hicho bila vikwazo.
Waziri Mkuu amewataka Wafamasia nchini kuzingatia maadili ya taaluma yao na kuhakikisha dawa zinatolewa kwa kufuata taratibu, ikiwa ni pamoja na kuto kutoa dawa bila cheti cha daktari, na ni jukumu la kila Mfamasia kuhakikisha dawa zinatolewa kwa kufuata taratibu sahihi.
“Kutoa dawa bila cheti cha daktari kunahatarisha maisha na kuharibu maadili ya taaluma hii muhimu, na pia wananchi wanatakiwa kuacha matumizi holela ya dawa na badala yake wafike katika vituo vya kutolea huduma za afya na kupima kisha kutumia dawa stahiki inayotakiwa badala ya kutumia dawa bila ya kujua nini tatizo,” amesisitiza.
#KAZIINAONGEA
No comments: