Madiwani Nanyamba Mtwara wakoshwa na miradi Mwanza
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nanyamba, Mhandisi Mshamu Munde amesema Halmashauri hiyo inatarajia kuanza utekelezaji wa miradi ya TACTIC ikiwemo ujenzi wa stendi ya mabasi, soko na dampo hivyo Halmashauri ya Jiji la Mwanza ni eneo sahihi la kujifunza utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo.
“Halmashauri yetu inategemea zao la korosho kama chanzo kikuu cha mapato hivyo tumekuja Mwanza kujifunza kuhusu uanzishaji na usimamizi wa miradi mipya ya soko, stendi na dampo ili kuongeza mapato ya Halmashauri” amesema Mwenyekiti Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, Kapende Abdallah.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Mazingira Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Desderius Pole akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo amesema hatua ya Halmashauri mbalimbali nchini kwenda kujifunza kwenye Jiji hilo inawakumbusha watumishi kuongeza juhudi zaidi katika utendaji kazi.
Pole ameongeza kuwa ili Halmashauri ziweze kuwa na uwezo wa kujiendesha na kutoa huduma bora kwa wananchi, zinapaswa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuvisimamia kwa njia shirikishi na kuhakikisha mapato hayapotei.
“Halmashauri nyingine zote, zinakaribishwa kuja kujifunza mema kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, pia nasi tuko tayari kuyapokea mema kutoka kwao” amesema Pole.
Ziara ya madiwani na waaalamu kutoka Halmashauri ya Nanyamba imetamatika kwa kutembelea vivutio vya utalii jijini Mwanza ikiwemo hifadhi ya Taifa Saanane pamoja na jiwe la ‘Bismack’ lililopo katika fukwe ya Kamanga.
Mradi wa stendi ya mabasi Nyegezi jijini Mwanza.
Eneo la fukwe kuelekea hifadhi ya Saanane jijini Mwanza.
Fukwe ya Kamanga jijini Mwanza yenye mawe ya kuvutia 'Bismack Rock'.
Tazama BMG TV hapa chini
No comments: