LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wenyeviti wa Mitaa Mwanza wapewa semina, watakiwa kujiepusha na migogoro

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi amewataka wenyeviti wa mitaa kujiepusha na utendaji kazi usiozingatia sheria, kanuni na taratibu hatua itakayosaidia kuepuka migogoro katika mitaa yao.

Makilagi ametoa rai hiyo Jumatano Disemba 18, 2024 wakati akifungua semina ya siku moja yaliyolenga kuwajengea uwezo wenyeviti wa mitaa 175 iliyoko kwenye Kata 18 za Halmashauri ya Jiji la Mwanza ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Alisema wenyeviti wa mitaa wanawaongoza wananchi katika shuguli mbalimbali za kijamii pamoja na kuwaletea maendeleo hivyo hawapaswi kuwa chanzo cha migogoro.

"Uongozi unahitaji busara na kuridhika na hali ya maisha uliyonayo kazi ya kuuza viwanja siyo kazi ya mwenyekiti wa mtaa,ndio maana huwa mnasababisha migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikileta kero kwa wananchi mnaowahudumia" amesema Makilagi.

Aidha ameongeza kuwa miongoni mwa kazi za wenyeviti wa mitaa ni kuibua miradi mbalimbali katika maeneo yao ambayo italeta tija kwa wananchi.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Witness Malero amewaomba wenyeviti kuwa waadilifu wanapowahudumia wananchi sanjari na kuzingatia maadili ya kazi.

Naye Mkurugenzi wa Tafiti, Shauri Elekezi na Mafunzo ya Muda Mfupi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Dodoma, Bahati Mfungo amesema semina hiyo ni muhimu kwa wenyeviti wa mitaa kwani itawasaidia kukumbuka majukumu yao ya kazi na kujifunza vitu vipya ambavyo vinakuwa vimebadilika ikiwemo sera na miongozo.

Kwa upande wake Machoke Mwita ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani na Zainabu Alphani wa Mtaa wa Karuta ambao ni miongoni mwa washiriki wa semina hiyo, wamesema itawasaidia kufanya kazi zao vizuri huku wakiahidi kushirikiana vyema na wananchi katika shughuli za maendeleo. 
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (aliyesimama) akizungumza kwenye semina hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Tafiti Shauri Elekezi na Mafunzo ya Muda Mfupi, Bahati Mfungo na kulia ni viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Wenyeviti wa Mitaa mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwa kwenye semina ya kujengewa uwezo.

No comments:

Powered by Blogger.