Jiji la Mwanza laimarisha huduma ya lishe kwa wanafunzi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Thomas Salala (kulia) akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Lishe kwa Robo ya Pili mwaka wa Fedha 2024/25. Kushoto ni Mganga Mkuu Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Dkt. Furaha Mwakafwila.
Halmashauri ya Jiji la Mwanza imejiimarisha katika utoaji wa huduma ya chakula shuleni hatua ambayo imesaidia kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi pamoja na kukabiliana na changamoto ya mdondoko wa wanafunzi hasa shule za msingi.
Miongoni mwa Kata zilizotajwa kufanya vizuri katika mpango huo ni Nyegezi ambayo imeendelea kutekeleza vizuri upatikanaji wa huduma ya chakula shuleni hatua na hivyo kuchochea ubora wa wanafunzi kujifunza pamoja na ufaulu kwa wanafunzi.
Hayo yamebainishwa Feburuari 04, 2024 katika kikao cha kamati ya lishe ngazi ya Wilaya ya Nyamagana kwa kipindi cha robo ya pili mwaka wa fedha 2024/25 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mtendaji wa Kata ya Nyegezi Shabani Mpuya alisema wazazi pia wamekuwa na mwitikio mzuri wa kuchangia chakula shuleni kwa wakati na hivyo kufanya mpango wa lishe kwa shule za msingi na sekondari kuimarika zaidi.
"Miongoni mwa shule ambazo watoto wanapata huduma ya chakula ni shule mpya ya msingi Swila na shule ya sekondari Nyabulogoya. Wazazi wanajitoa vizuri kwani tumekubaliana kuanzia darasa la tatu hadi la tano wanachangia shilingi 500 kila siku na darasa la sita hadi la saba ni 1000 na wazazi wanatoa fedha hizo kwa wakati" alisema.
Aidha alisema endapo kuna changamoto katika shule ambazo ziko kwenye Kata nyingine waende wajifunze kwenye Kata ya Nyegezi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Dkt. Furaha Mwakafwila alisema katika kikao hicho wameazimia kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni kwa kuendelea kuihamasisha jamii umuhimu wa watoto kula shuleni.
Alisema wazazi wanapaswa watambue umuhimu wa watoto wao kula chakula shuleni kwani inasaidia kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana, Thomas Salala ambaye alikuwa anaongoza kikao hicho alisema takwimu zinaonesha kwa upande wa shule za msingi suala la lishe liko asilimia 49 huku sekondari ikiwa ni asilimia 53.
Alisema wazazi wanahimizwa kuchangia chakula shuleni hasa katika Kata za Kata ya Igogo na Isamilo ambazo zimeonekana kuwa na mwitikio mdogo wa uchangiaji.
"Tumejipanga kufanya vikao na kamati za shule ili tuweze kukubaliana mbinu za kuendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa chakula shuleni. Tunakusudia kupanda angalau kwenye shule za msingi tufike asilimia 80 na sekondari asilimia 90" alisema Salala.
Imeandaliwa na Hellen Mtereko, Mwanza
No comments: