DC Nyamagana awatoa hofu wananchi adha ya maji
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wananchi wa Mtaa wa Nyamazobe, Kata ya Mkolani Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, wamemuomba Mkuu wa Wilaya hiyo- Amina Makilagi kuwatatulia kero ya maji safi na salama ambayo imekuwa ni ya muda mrefu.
Ombi hilo wamelitoa Machi 28, 2025 wakati walipokuwa wakiwasilisha changamoto mbalimbali ikiwemo ya maji kwa Mkuu huyo wa Wilaya ambaey alifanya ziara katika Kata hiyo kwa kengo la kusikiliza kero za wananchi ili kutafutiwa ufumbuzi.
Walisema kwa sasa hawana huduma ya uhakika ya maji kutokana na kupata maji mara moja kwa wiki hivyo wakaomba watizamwe kwa jicho la tatu kwani wamekuwa wakipata shida sana.
"Maji yanatoka mara moja kwa wiki au muda mwingine hata hiyo wiki yanaweza yasitoke tunalazimika kununua maji kwa gharama kubwa kutoka katika maeneo jirani jambao ambalo kwa baadhi ya watu imekuwa ni ngumu kumudu gharama za ununuzi wa maji" walisema.
Walisema wamezungukwa na Ziwa Victoria lakini kupata maji ya uhakika kwao imekuwa histori hivyo wanajiona kama wako kisiwani kutokana na kukosa huduma hiyo muhimu ya maji.
Akizungumza na wananchi hao,bMakilagi alisema Serikali imetoa bilioni 46 kwa ajili ya kujenga matenki katika mitaa minne na kusambaza mabomba.
"Mtaa wa Nyamazobe litajengwa tenki la lita milioni tano na litasambaza maji katika Mitaa ya Kata ya Mkolani, Sahwa litajengwa la lita milioni 10, Buhongwa Lita milioni 10 na Fumagila lita milioni 10" alisema Makilagi.
Alisema katika ujenzi wa matenki hayo umeshaanza kutekelezwa katika mitaa miwili ambayo ni Buhongwa na Sahwa.
"Nyamazobe na Fumagila ujenzi haujaanza kutokana na wananchi waliopitiwa na ujenzi wa mradi huo kusubiri fidia zao" alisema Makilagi.
"Tenki hili linalojengwa katika Mtaa wenu wa Nyamazobe na litakuwa suluhisho la kero ya maji safi na salama inayowakabili" alisema Makilagi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usambazaji Maji kutoka Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA), Celestine Mahubi alisema wananchi waliopitiwa na mradi huo ni 36 hivyo wanasubiRi walipwe fidia ili mkandarasi aanze kazi.
Wananchi wakifuailia mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi.
Tazama BMG TV hapa chini, ziara ya Makilagi Kata ya Mbugani.
No comments: