LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Nyamagana azindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria, ataka isaidie kutatua migogoro

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amezindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria wilayani humo na kuitaka kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma hasa utatuzi wa migogoro ya wananchi.

Makilagi amefanya uzinduzi huo Jumanne Machi 25, 2025 jijini Mwanza na kubainisha kuwa kamati hiyo inatakiwa kutekeleza majukumu yake ya kusikiliza malalamiko ya kisheria na kutoa elimu kwa umma.

Aidha ameitaka kuhakikisha inapokea malalamiko, migogoro na kuifuatilia mpaka mwisho ili kujiridhisha ni kwa namna gani imemalizika na kuweka kumbukumbu ya kufungua na kufunga migogoro hiyo.

"Lengo la kuweka kumbukumbu ni kuzuia walalamikaji kurudi baadaye kuwasilisha malalamiko yaliyopita hasa pale wanapoona uongozi umebadilika" alisema Makilagi

Akizungumzia suala la kutoa elimu kwa umma, Makilagi alisema ni endelevu na siyo lazima lisubiri kamati hiyo huku akiielekeza kamati hiyo kuendelea kushirikiana na kuwahudumia wananchi kwa kutoa ushauri stahiki.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Nuru Mwambuli alisema kamati hiyo itakuwa ni msaada katika kuwafikia wananchi, viongozi na watumishi wa umma kwa ajili ya kutoa ushauri wa kisheria.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Wilaya ya Nyamagana, Wakili Naila Chamba alisema atashirikiana na taasisi mbalimbali za kiserikali kutekekeza jukumu la kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Mkolani jijini Mwanza, Dioniz Swalala alisema uwepo wa kamati hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua malalamiko ya wananchi.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akizungumza kwenye uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria katika wilayani humo.
Wakili wa Serikali Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Nuru Mwambuli (kulia) akikabidhi kitabu cha miongozo kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (kushoto). Kulia ni Diwani wa Kata ya Mkolani, Dioniz Swalala.
Wakili wa Serikali Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Nuru Mwambuli akizungumza kwenye uzinduzi wa Kamati ya Ushauru wa Kisheria ngazi ya Wilaya ya Nyamagana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria Wilaya ya Nyamagana, Wakili Naila Chamba akizungumza kwenye uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Wilaya ya Nyamagana.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Wilaya ya Nyamagana.

No comments:

Powered by Blogger.