Serikali ya Rais Samia yatoa maelekezo kwa Wauguzi, Wakunga
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Afya imefanya mapinduzi makubwa katika kuboresha huduma za afya kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya majengo, vifaa tiba, upatikanaji wa dawa pamoja na watumishi.
Katika kuhakikisha jamii inapata huduma bora ya afya, Waziri wa Afya Jenista Mhagama amewataka wauguzi na wakunga viongozi kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinaanzisha na kuimarisha madawati ya huduma kwa mteja ili kuhakikisha kero za wananchi vituoni zinashughulikiwa kwa wakati na kupatikana kwa mrejesho haraka.
Waziri Mhagama alitoa maelekezo hayo Machi 28, 2025 wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa wauguzi viongozi uliofanyika mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, waganga wafawidhi wa hospitali za mikoa, wasajili wa mabaraza pamoja na wadau wa maendeleo.
"Nawataka pia, mkafuatilie na kuhakikisha wateja wanapata huduma kwa wakati na kutoa elimu, kwani ni wajibu wa mteja na mtoa huduma, kuimarisha usimamizi wa ndani wa utoaji huduma sambamba na kuimarisha matumizi ya miongozo kwenye utoaji wa huduma kwa kuhakikisha usalama kwa wateja" alisema Waziri Mhagama.
Aidha Waziri Mhagama aliwataka wauguzi viongozi hao kuendelea kusimamia taaluma yao, nidhamu, maadili na ubunifu katika kazi ili kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma bora za afya na zenye staha pamoja na utu kwa kuzingatia usiri baina ya mgonjwa na mtoa huduma.
"Kipaumbele chetu kikubwa kwa sasa kama Wizara ya Afya ni kuimarisha usimamizi wa utoaji wa huduma bora za afya na utendaji kazi wa watumishi mnaowasimamia, ninyi ndio wasimamizi wa nguvu kazi ya sekta ambao wanatoa huduma kwa takribani asilimia 80, niwasihi sana mkayatekeleze kwa ufanisi haya yote mliyoazimia ili kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma za afya nchini" alisema Waziri Mhagama
"Ndugu zangu wauguzi na wakunga viongozi, nawahakikishia kuwa Wizara ya Afya itaendelea kufanya kazi bega kwa bega nanyi ili kuboresha na kusimamia mifumo ya utoaji wa huduma za afya katika ngazi zote, kwa pamoja, tunaweza kubuni sera na taratibu ambazo zitahakikisha uuguzi na ukunga unakuwa ni chaguo endelevu kwa vizazi vijavyo" alisema Waziri Mhagama.
Kazi Inaongea!
Kazi na Utu, Tunasonga Mbele
No comments: