LIVE STREAM ADS

Header Ads

INEC Yatambua Nguvu ya Makundi Maalum Katika Mafanikio ya Uchaguzi Mkuu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Na Cathbert Kajuna – Dar es Salaam.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) yatoa wito mpya: “Tumia sauti yako, hamasisha ushiriki!”

Katika kilele cha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevitaka vikundi mbalimbali vya kijamii kutumia majukwaa yao kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi kwa njia ya amani na uwajibikaji.
Wito huo umetolewa leo, Julai 31, 2025, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele, wakati wa kufungua mkutano kati ya Tume na wawakilishi wa watu wenye ulemavu.

“Tume inatambua nafasi yenu katika jamii. Tunawaomba kuwa mabalozi wa amani, kusambaza taarifa sahihi na kuwahimiza wenzenu kushiriki uchaguzi bila jazba wala chuki,” alisema Jaji Mwambegele.

Ameeleza kuwa Tume itaendelea kushirikiana na makundi hayo katika hatua zote muhimu kuelekea uchaguzi, huku akibainisha kuwa ratiba rasmi ya uchaguzi tayari imetangazwa: utoaji wa fomu kuanzia Agosti 9 hadi 27, 2025, na kampeni rasmi kuanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 kwa Tanzania Bara.
Katika mkutano tofauti uliofanyika pia jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mbarouk Salim Mbarouk, amewahimiza wanawake kuwa mstari wa mbele katika kueneza taarifa sahihi kuhusu maandalizi ya uchaguzi, na kuhamasisha waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi.
“Tunawapongeza wanawake kwa ushirikiano mkubwa mlioonesha wakati wa uboreshaji wa daftari. Endeleeni kuwa chanzo cha matumaini kwa jamii,” alisema Jaji Mbarouk.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume, Mheshimiwa Jaji Asina Omari, ametoa tahadhari kwa vijana kuhusu matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, akisisitiza umuhimu wa kutumia majukwaa ya kidijitali kwa uadilifu.
“Vijana mnao uwezo mkubwa wa kuathiri mwelekeo wa uchaguzi. Tumia mitandao kwa njia chanya. Jiepusheni na upotoshaji, uchochezi na matumizi mabaya ya teknolojia mpya kama akili bandia (AI),” alionya Jaji Asina.

Tume ya Uchaguzi imeendelea kusisitiza kwamba uchaguzi wa mwaka huu unapaswa kuwa wa heshima, haki, na mshikamano. Kauli mbiu ya Tume ni “Kura Yako, Haki Yako – Jitokeze Kupiga Kura” ikiwa ni wito kwa Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika kudumisha demokrasia ya kweli.

No comments:

Powered by Blogger.