Wanafunzi wa Misri wazindua mpango wa kipekee wa Diplomasia ya Afya
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Kwa mara ya kwanza barani Afrika, wanafunzi wa Misri wamezindua Mpango wa “Diplomasia ya Afya kwa Wanafunzi wa Tiba”, hatua ya kipekee inayolenga kuwajengea uwezo madaktari chipukizi kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya maamuzi ya kisera ya afya kitaifa na kimataifa.
Uzinduzi huo umefanyika kwa udhamini wa Muungano wa Kimataifa wa Wanafunzi wa Tiba – Misri, kupitia tawi lake katika Chuo Kikuu cha MTI, kwa ushirikiano na Jumuiya ya Kisayansi ya Wanafunzi wa Tiba wa Chuo Kikuu cha Kisasa cha Teknolojia na Habari (MTI University), huku ukipata ufadhili wa bure wa matangazo kutoka Mpango wa Afromedia wa Mawasiliano na Uandishi wa Habari kwa Maendeleo.
Kwa kuzingatia hali ya vita nchini Sudan, mpango huu umewajumuisha pia wanafunzi wa Sudan walioko Misri, wakiwemo wakimbizi, kwa lengo la kuwapatia mazingira jumuishi ya elimu na uzoefu wa vitendo vinavyoweza kuwajengea msingi wa ushiriki hai katika maendeleo ya jamii kupitia sekta ya afya.
Mpango huu umebuniwa kwa njia ya ubunifu ili kuwawezesha wanafunzi kuelewa kwa kina masuala ya afya ya umma, diplomasia ya afya, sera za afya barani Afrika, na fursa za kimataifa za kujitolea katika taasisi za afya. Aidha, unaweka msisitizo juu ya umuhimu wa daktari si kama mtoa huduma tu, bali pia kama kiongozi, mtafiti, mpatanishi, na mshawishi wa sera.
Katika mpango huu, watoa mada mashuhuri kutoka sekta mbalimbali walishiriki, akiwemo Bw. Mostafa Magdy, Msaidizi wa Waziri wa Vijana na Michezo; Dkt. Samah Kamel wa Umoja wa Mataifa; Dkt. Mahmoud Al-Qally, mkufunzi wa maendeleo endelevu; na Dkt. Ahmed Al-Rifai, mtaalamu wa siasa za kimataifa. Wengine ni Dkt. Dalia Ghazlan (mtaalamu wa elimu ya afya), Hamada Qaoud kutoka Taasisi ya Taifa ya Utawala, Ahmed Abu Douma kutoka Jukwaa la Vijana wa Kiarabu, na Dkt. Rumaila Shahir wa Chuo cha Kijerumani, Kairo.
Miongoni mwa waliochangia kwa kina ni Hassan Ghazaly, mtafiti wa anthropolojia na mwanzilishi wa Mtandao wa Mshikamano wa Kimataifa, ambaye alieleza umuhimu wa taaluma ya anthropolojia katika kusaidia madaktari kuelewa jamii wanazotoa huduma. Pia alifafanua nafasi ya diplomasia ya umma na fursa za madaktari wa Kiafrika katika ajenda za afya za bara kupitia serikali ya Misri na Umoja wa Afrika.
Katika hotuba yake ya shukrani, Ghazaly aliwatambua Prof. Mohy El-Din Ragab El-Banna (Mkuu wa Chuo cha Tiba) na Prof. Hisham Mohamed Omran (Naibu Mkuu wa Chuo) kwa mchango wao wa kipekee katika kuwezesha na kuunga mkono ushiriki wa wanafunzi wa Kiafrika ndani ya taasisi za elimu ya juu nchini Misri.
Mpango huu ni sehemu ya mkakati mpana wa kubadili mwelekeo wa elimu ya tiba kutoka mtazamo wa kitaaluma pekee kuelekea ushiriki wa kijamii na majukumu ya kidiplomasia. Unalenga kuzalisha kizazi kipya cha madaktari walioko mstari wa mbele si tu katika hospitali, bali pia kwenye meza za maamuzi ya sera na maendeleo ya jamii.
Waandaaji wamesisitiza kuwa uzinduzi huu ni mwanzo tu wa mlolongo wa matoleo yanayokuja, yakilenga kuifanya Misri kuwa kitovu cha diplomasia ya afya barani Afrika.
Mwanzilishi wa Jukwaa la Nasser, Dkt. Hassan Ghazaly.
Imeandaliwa na Mtafiti wa Kiswahili, Mervat Sakr ambaye pia ni Mratibu wa Lugha ya Kiswahili katika Jukwaa la Kimataifa la Nasser.
PIA>>> Bonyeza hapa kusoma zaidi
No comments: