LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watendaji Kata, Maafisa Tarafa Kanda ya Ziwa wapewa mafunzo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, ubunifu na ufanisi ili kuleta tija katika jamii.

Mtanda alitoa wito huo Julai 29, 2025 wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Watendaji wa Kata 222 na Maafisa Tarafa 21 kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Geita, Tabora na Kagera.

Mafunzo hayo yalianza Julai 2024 kwa lengo la kuwajengea uwezo katika usimamizi na uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

“Kazi yako ukiipenda utafanya juhudi, na ukifanya hayo basi utajikuta umejiendeleza kielimu, kuweka weledi na nidhamu” alisema Mtanda.

Aidha aliwasisitiza kutumia taaluma zao kuonyesha tabia njema kwa jamii, kufanya maamuzi yanayozingatia Sheria, Kanuni na miongozo ya sekta husika, hasa katika masuala nyeti kama ardhi, huku akipinga vikali vitendo vya upendeleo au uonevu vinavyoweza kuharibu utendaji kazi.

Pia aliwataka viongozi hao kwenda kuwaunganisha wananchi badala ya kuwagawanya, huku wakihamasisha ushiriki wao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ujenzi wa madarasa, barabara na miradi ya maji.

Alisisitiza umuhimu wa viongozi hao kuishi kwa kuendana na mazingira ya wananchi wanaowaongoza, kuwa wabunifu kwa kubaini vyanzo vipya vya mapato na kuviwasilisha kwenye halmashauri husika ili viweze kuingizwa kwenye mipango ya kodi na ushuru.

Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Jonas Kapwani alieleza kuwa washiriki walipata uelewa wa kina kuhusu muundo na majukumu yao ya kikazi, Sera na Sheria za Serikali, mbinu za kusimamia miradi ya maendeleo, namna ya kushughulikia kero za wananchi kwa wakati na usimamizi bora wa rasilimali na mapato ya ndani.

Kapwani alieleza kuwa mafunzo hayo pia yalijumuisha mada kuhusu uongozi, utawala bora, matumizi sahihi ya fedha za umma, ununuzi wa bidhaa kwa mujibu wa sheria, maadili ya utumishi wa umma na utunzaji wa siri za Serikali.

Washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuwa yamewajengea uwezo mkubwa katika utendaji wao wa kazi na yatawasaidia kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.
Na Chausiku Said, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.

No comments:

Powered by Blogger.