WACHIMBAJI WADOGO GEITA KUKAMILISHA UJENZI WA ZAHANATI ULIOKWAMA MIAKA 10
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wachimbaji wadogo wa mgodi katika Kijiji cha Msasa, Kata ya Runzewe-Magharibi Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamejitolea kukamilisha Zahanati ya Kijiji hicho iliyokwama kwa zaidi ya miaka 10.
Mkurugenzi Mtendaji wa mgodi wa Msasa, Cosmas Ignasi alitoa taarifa hiyo mbele ya viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Msasa waliotembelea na kukagua maendeleo ya Zahanati hiyo.
Ignasi alisema uongozi wa mgodi huo umeamua kuikamilisha Zahanati hiyo ili kukabiliana na changamoto iliyopo ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika Vijiji vya Kata jirani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Msasa, Tulinge Paschal alisema ujenzi wa Zahanati hiyo ulianza miaka 10 iliyopita kupitia nguvu za wananchi kuanzia hatua ya msingi mpaka ujenzi wa boma hivyo mgodi wachimbaji wadogo kuwashika mkono utaondoa adha kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya kijijini hapo.
Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho walisema, wajawazito wengi walikuwa wanashindwa kuhudhuria kliniki kutokana na huduma za afya kupatikana mbali.
Walisema Zahanati hiyo itakapokamilika itapunguza adha ya akina mama, wazee na watoto kufuata huduma za afya umbali mrefu katika Kata ya Unyovu.




No comments: