LIVE STREAM ADS

Header Ads

BALOZI MSTAAFU WA TANZANIA NCHINI UINGEREZA NA MAREKANI AONGOZA ZOEZI LA UWEKAJI MASHADA YA MAUA KATIKA MAKABURI YA KUMBUKUMBU YA AJALI YA MELI YA MV.BUKOBA.

Manusura wa ajali hiyo, Ndugu, Jamaa na Marafiki wasikitishwa na Kusahaulika kwa Makaburi hayo yaliyoko Igoma Jijini Mwanza, Mwanamitindo Flavian Matata Aguswa na hali hiyo.

Balozi wa Mwanaidi Majaar watatu waliokaa kutoka Kulia.
Balozi Mstaafu wa Tanzania nchini Uingereza na Marekani Mwanaidi Majaar jana ameongoza zoezi la Kuweka Mashada katika Makaburi ya Kumbukumbu ya Watu waliopoteza Maisha katika ajali ya Meli ya Mv.Bukoba iliyotokea May 21 Mwaka 1996 Mkoani Mwanza ikitokea Bukoba Mkoani Kagera.
  
Zoezi la Kuweka Mashada hayo lilitanguliwa na Ibada maalumu ya Kuwaombea Marehemu waliotangulia mbele za haki katika ajali hiyo, ambapo Viongozi wa dini ambao ni Sheikh, Padri na Mchungaji waliongoza Ibada hiyo ambapo zaidi walisisitiza kwamba ni jambo jema na la wajibu kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliotangulia mbele za haki.
Balozi Majaar, ndugu, jamaa na marafiki wakiweka mashada ya maua.
Akizunguza Mara baada ya Ibada hiyo, Balozi Majaar ambae alifika katika makaburi hayo na kushiriki shughuli zote za kumbukumbu ya Miaka 18 tangu kuzama kwa Meli ya Mv.Bukoba kwa Mwaliko wa Mwanamitindo Maarufu nchini ambae pia anafanya shughuli zake Barani Ulaya Flavian Matata, Alisema kuwa kumbukumbu ya ajali hiyo itumike kama tafakari ya kuhakikisha kwamba maisha ya watu hayapotei bila sababu ama kutokana na uzembe wowote ule.


Aidha aliwasihi wale wote wanaohitaji kuweka kumbukumbu ya Kudumu katika Makaburi hayo yaliyoko Igoma Jijini Mwanza, kujitokeza na kuungana kwa pamoja katika kuyafanyia ukarabati badala ya kuiachia Serikali ama Halimashauri ya Jiji.

  
Kwa Upande wake Flavian Matata ambae katika ajali hiyo alimpoteza mama yake mzazi sanjari na binamu yake, amewashukuru watu wote waliohudhuria katika kumbukumbu hiyo ya Ajali ya Mv.Bukoba ambapo amesisitiza kwamba jambo kubwa zaidi ni kuwaombea wale wote waliopoteza maisha wapumzike kwa amani.


Aidha kutokana na hali ya Makaburi hayo kutokuwa katika hali nzuri hususani kutofanyiwa usafi wa mara kwa mara, Matata aliahidi kulishughulikia suala hilo huku akibainisha kuwa tayari ana mpango wa kufanya ukarabati katika eneo hilo ambapo tayari mipango ya ukarabati huo imekwisha kuanza.
Mwanamitindo Flavian Matata (aliesimama mwenye miwani) ameahidi kufanya ukarabati katika makaburi hayo.
Baadhi ya Manusura, Ndugu, jamaa na marafiki wa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo walishauri Serikali kuweka uangalizi mzuri katika makaburi hayo badala ya kuwa kama yametelekezwa kwa kuweka utaratibu wa kuyafanyia usafi wa mara kwa mara sanjari na kuyafanyia ukarabati.
  
Aidha waliiomba Serikali kuvifanyia ukaguzi vyombo mbalimbali vya usafiri hapa nchini hususani vile vya majini kwa kuwa asilimia kubwa ya vyombo hivyo havikaguliwi na viko katika hali inayohatarisha maisha ya abiria wanaovitumia. Likiwa ni suala ambalo pia amelielezea Mwanamziki Ambwene Yesaya Maarufu kama AY ambae pia amehudhuria kumbukumbu hiyo ya Mv.Bukoba.
Mwanamziki Ambwene Yesaya maarufu kama AY nae alikuwepo.
Meli ya Mv.Bukoba iliyoundwa mwaka 1979 ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 850 na abiria 430 ilizama katika Maji ya Ziwa Victoria Mkoani Mwanza ikiwa ni kilomita chache tu kutoka ufukweni mwa maji na kusababisha zaidi ya watu 1,000 kumepoteza maisha katika Meli hiyo ambayo tangu kuundwa kwake hadi kuzama kwake ilikuwa na umri wa miaka 17.Hata hivyo maswali mengi yalibaki vichwani mwa watu wengi kutokana na idadi ya abiria waliofariki katika ajali hiyo ukijumuisha na waliookolewa, kulinganisha na uwezo wake wa kubeba abiria. 

No comments:

Powered by Blogger.