LIVE STREAM ADS

Header Ads

BOMOA BOMOA KATIKA MTAA WA MAKOROBOI JIJINI MWANZA YASABABISHA TAHARUKI KWA TAKRIBANI MASAA MANNE. MSIKITI WA WAHINDI NUSRA UCHOMWE MOTO. SOMA NA TAZAMA KILICHOJILI.

Kikosi cha zima moto kikizima moto ambao uliwashwa pembezoni mwa msikiti wa Shree Akshar Purushottam Swaminarayan Tempe maarufu kama Msikiti wa Wahindi ulioko mtaa wa Makoroboi ambako leo bomoa bomoa imefanyika na kuhatarisha usalama wa Jiji la Mwanza.
Nusra Msikiti huu uungue kwa moto, baada ya mbao zilizokuwa zimewekwa eneo hili kuchomwa moto na baadhi ya vijana ambao walikuwa wanapinga kuondolewa katika eneo hili la Makoroboi.
Hali ilikuwa tete kwa zaidi ya masaa manne yaliyopita, hali bado si nzuri katikati ya jiji la Mwanza, Kinachisikika ni Mabomu ya kutoa machozi kwa ajili ya kutawanya wananchi waliokusanyika mitaani, wengi wao wakiwa ni wale wanaofanya biashara ndogo ndogo katika Mtaa wa Makoroboi.
Hili ni eneo ambalo bomoa bomoa imefanyika ambalo liko katika Mtaa wa Makoroboi Jijini Mwanza. Eneo hili kulia na kushoto kulikuwa na vibanda vya wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga.
Geti la kuingilia Msikitini, ambapo barabara ya kuingilia na kutokea katika Msikiti huu imebaki wazi baada ya safisha safisha kufanyika katika Mtaa huu wa Makoroboi. Bomoa bomoa hii haijayajumuisha maeneo yote ya Mtaa wa Makoroboi, ila imewalenga wale waliokuwa wanafanyia biashara zao katika eneo la kuingilia na kutokea katika Msikiti wa huu ambao unafahamika kama Msikiti wa Waarabu ambao uko katikati ya Mtaa wa Makoroboi.
Vijana ambao wanafanyia biashara zao katika Mtaa wa Makoroboi wakijadiliana mara baada ya mabanda yao ya biashara kubomolewa. Baada ya hapa kilichofuatia ni kuanza kuchoma moto eneo la Msikiti ambako kulikuwa kumekusanywa mbao na mabanda yaliyobomolewa.
Mbao zilizobomolewa kabla ya kuchomwa moto na baadhi ya machinga
Barabara ya kuingia na kutoka eneo la Msikiti wa Wahindi katikati ya Mtaa wa Makoroboi mara baada ya bomoa bomoa.
Ndivyo ilivyokuwa wakati wa zoezi la ubomoaji wa vibanda vya wafanyabiashara ambao wanafanyia biashara zao eneo ambalo inadaiwa kuwa haliruhusiwi kwa ajili ya biashara.
"Sisi hapa wametubomolea kwa makosa, sisi hatukupaswa kubomolewa" Mmoja wa mtu mwenye duka amesikika akisema hivyo katika uchochoro huu ambao uko pembezoni kabisa na barabara inayoingia na kutoka katika Msikiti huo wa Wahindi.
Kwa wenzetu ambao wako jirani na Msikiti wa Waarabu hali ilikuwa tofauti, wao walikuwa wakishangaa namna Mwanza ilivyogeuka kuwa Mogadishu, baada ya polisi wa kutuliza ghasia (FFU) kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafanyabiashara ambao walianza kuandamana na kuwasha moto vitu mbalimbali katika Mtaa wa Makoroboi.
Hadi Mtanzania Media inaondoka eneo la Makoroboi na maeneo jirani yaliyoko katikati ya jiji la Mwanza, hali ilikuwa ni tete baada ya Makundi ya wafanyabiashara ndogo ndogo kuzagaa mitaani wakipinga kubomolewa kwa mabanda yao katika eneo la Msikiti wa Shree Akshar Purushottam Swaminarayan Tempe maarufu kama Msikiti wa Wahindi uliopo mtaa wa Makoroboi.

Maaskari wa kutuliza ghasia FFU walikuwa bado wakiendelea na juhudi za kutuliza ghasia ambazo zilikuwa zimeanza kufanywa na baadhi ya machinga katika Mtaa wa Makoroboi ambako alfajiri ya leo imefanyika bomoa bomoa.

"Sisi tunashangaa kwanini wanakuja kutubomolea mabanda yetu ya kufanyia biashara tena bila taarifa, ni bora wangetupa taarifa. Tuna watoto tunasomesha sasa tutawasomeshaje? hapa nilipo kama mimi sijui nitafanyaje, jana nimechukua mkopo bank na nategemea biashara hii ndogo ndogo kwa ajili ya kurejesha huo mkopo, sasa walivyotubomolewa wanategemea nini, hatukubali hatukubali kamwe..." Alisema mmoja wa machinga ambe alikumbwa na bomoa bomoa hiyo.

Baada ya bomoa bomoa hiyo kufanyika alfajiri ya hii leo, machinga walioko Makoroboi walianza kufanya fujo na hivyo kusababisha shughuli zote katikati ya jiji la Mwanza kusimama hadi hivi sasa majira ya saa saba za mchana, huku jeshi la polisi likitumia zaidi ya masaa matatu kupambana na machinga hao kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.

"Mimi nawaomba hawa vijana wajaribu kuwa watulivu, hili suala tutakaa na viongozi wao tutazungumza ili tuone namna ya kufanya ili tuhakikishe hawa vijana wanatafuta riziki, mimi nilisikia kutoka kwa Mkuu wa Mkoa kwamba chanzo ni wahindi wanalalamika kwa hiyo mimi kama mlezi nitaenda nipige magoti kwa wahindi kwamba hakuna njia mwafanya ya kufanya ili vijana waendelee kutafuta riziki, kwa hiyo majibu nitayapata kutoka kwa wahindi, hakuna kinachoshindikana kwa hiyo nawaomba vijana wawe watulivu" Alisema Mlezi wa Machinga Mkoa wa Mwanza Alfred Wambura mara baara ya bomoa bomoa hiyo, zikiwa ni dakika chache kabla ya kuibuka kwa taharuki katika Mtaa wa Makoroboi. 

Mpaka sasa hakuna mamlaka yoyote ambayo imetoa taarifa sahihi juu ya usahihi wa kuwepo machinga katika mtaa huo wa Msikiti wa Wahindi uliopo Makoroboi ama laa, japo machinga walioko katika eneo hilo wanasema wao kufanyia biashara mkabara na msikiti huo hakuoathiri chochote.Viongozi wa Machinga hawakuweza kupatikana hata baada ya kupigiwa simu zilikuwa hazipokelewi ili kutoa ufafanuzi juu ya suala hii, huku pia juhudi za kuwatafuta viongozi wa halmashauri ya jiji la Mwanza nazo zikigonga mwamba kwa madai kwamba wako nje ya ofisi kwa ajili ya vikao vya dharura. Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza Valentino Mlowola hakuweza kuzungumzia operation hiyo kwa madai kuwa yuko Jijini Dar es salaam.

No comments:

Powered by Blogger.