ASKARI WA USALAMA BARABARANI MKOANI MWANZA WALALAMIKIWA. MADUDU WANAYOFANYA YAANIKWA WAZI.
Dereva Akielezea Kero anazozipata kutoka kwa Maaskari wa Usalama Barabani Mkoani Mwanza. |
Madereva
walioelezea Kukerwa na Tabia za baadhi ya Askari hao ni wale wanaofanya Safari
zao Kuanzia Nyegezi, Buhongwa Wilayani Nyamagana kwenda Ishokera, Misasi,
Sarawe hadi Wilayani Misungwi ambapo wamebainisha kuwa Maaskari wa Usalama
barabarani katika maeneo hayo wamekuwa na Utendaji kazi Mbovu ambao hauzingatii
sheria na kanuni zinazowaongoza.
Dereva Akielezea Kero anazozipata kutoka kwa Maaskari wa Usalama Barabani Mkoani Mwanza. |
Wakitoa
Malalamiko hayo hii leo katika Vituo vyao vya kazi vilivyopo Buhongwa na
Nyegezi Wilayani Nyamagana, Madereva hao wameeleza kuwa baadhi ya Maaskari wa
Usalama barabara katika Barabara ya Misungwi wamekuwa na tabia ya
kuwabambikizia makosa na kuwatoza faini kinyume na taratibu.
Aidha
wamebainisha kuwa Maaskari hayo wameanzisha utaratibu wa Kuwatoza shilingi Elfu
Tano (5,000) kila siku kwa madai ya magari yao kutokukaguliwa na ikiwa dereva
atakaa kutoa kiasi hicho hutafutiwa kosa lolote na hatimae kutozwa faini ambayo
hufikia hadi shilingi Elfu Thelathini (30,000).
Dereva Akielezea Kero anazozipata kutoka kwa Maaskari wa Usalama Barabani Mkoani Mwanza. |
“Hawa
maaskari wanapokezana kusimamisha Magari na kututafutia makosa. Ukionekana
kuwasumbua unaambiwa siku hizi umekuwa mjanja hutaki kujiunga na sisi. Kujiunga
kwenyewe unaambiwa utoe shilingi Elfu tano kila siku ili gari lako lisikagulie
na ukikataa kama huna kosa wanakuacha unaondoka na wanapiga simu unakamatwa kwa
mbele unaambiwa unaendesha gari kwa Speed (mwendo Kasi) na unaandikiwa faini”
Alieleza mmoja wa Madereva hao ambae anafanya safari zake za Nyegezi, Misungwi,
Misasi na Sarawe.
“Tabia hii
ya Kutoa Shilingi Elfu Tano kila Siku ambayo wenyewe wanaiita Cheka Time
imekuwa ni Suala endelevu. Binafsi sijafurahia vitendo wanavyovifanya” Alieleza
dereva mwingine ambae yeye anafanya safari zake za Buhongwa Wilayani Nyamagana kwenda
Misasi Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Dereva Akielezea Kero anazozipata kutoka kwa Maaskari wa Usalama Barabani Mkoani Mwanza. |
Akizungumzia
kero zilizotewa na Madereva hao, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Kanda ya Ziwa
(Victoria Drivers Assosiation) Dede Petro Dede ameeleza kuwa kero zote
zilizotolewa na madereva hao zinafanyiwa kazi na tayari viongozi wa chama hicho
sanjari na baadhi ya madereva wamekutana na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama
barabarani Mkoani Mwanza ili kujadili namna ya kuondoa kero hizo kwa madereva.
“Hizi kero
zinafanyiwa kazi. Kesho (Alhamisi) Madereva hawa walikuwa wamepanga kugoma,
lakini sisi kama uongozi tukasema hapana haiwezekani wananchi (abiria) wapate
shida ya usafiri kwa sababu ya watu wachache. Kwa hiyo tumekutana na Jeshi la
Polisi Kikosi cha Usalama barabari na tumezungumzia suala hili na tutakutana
tena katika kikao cha pili kwa ajili ya kuhakikisha kero hizi zinaondolewa na
madereva wanafanya shughuli zao kwa mjibu wa sheria na taratibu” Alisema Dede
na kuongeza...
“Kila siku
kukamatwa. Usipojiunga kutoa elfu tano unakamatwa na kuambiwa utoe shilingi
elfu thelathini. Huu ni ujanja wa baadhi ya watu kutaka kuichafua Serikali.
Tunaomba hii Serikali sikivu iwaangalie hawa Maaskari. Kwanza wamekaa katika
hii barabara ya Misungwi kwa muda mrefu, wabadilishwe maana wamezoeleka…”
Dereva Akielezea Kero anazozipata kutoka kwa Maaskari wa Usalama Barabani Mkoani Mwanza. |
Akizungumzia
kero zinazolalamikiwa na Madereva hao katika Kipindin cha Metro Evening Drive
Kinachorushwa na Metro FM Jijini Mwanza, Dede alieleza kuwa kitendo cha
maaskari wa usalama barabarani kupokea pesa kutoka kwa madereva ili magari yao
yasikaguliwe ni hatari kwa kuwa kuna baadhi ya madereva hawana leseni hivyo
wanaweza kuwa wanatoa pesa na kubeba abiria jambo ambalo linahatarisha usalama
wa abiria.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Kanda ya Ziwa Dede Petro Dede akizungumza na Madereva baada ya kueleza kero zao katika eneo la Nyegezi. |
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Kanda ya Ziwa Dede Petro Dede akizungumza na Madereva baada ya kueleza kero zao katika eneo la Buhongwa. |
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Kanda ya Ziwa Dede Petro Dede akizungumza na Madereva baada ya kueleza kero zao katika eneo la Buhongwa. |
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Kanda ya Ziwa Dede Petro Dede akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini Kwake. |
Na: George Binagi @Radio Metro & Mtanzania Media
No comments: