LIVE STREAM ADS

Header Ads

SOMA KWA UMAKINI MKUBWA SANA!

Kilimo ndiyo Sekta ambayo bado inaongoza hapa nchini kwa kutoa nafasi nyingi za ajira kwa Watanzania. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba
sekta ya Kilimo inaonekana kuwa ni sekta ya mwisho miongoni mwa wanajamii katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo.

Tofauti na Sekta nyingine, bado wakulima hapa nchini wanaishi katika mazingira magumu licha ya juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikielezwa na serikali pamoja na mashirika binafsi.Hivyo usishangae kukutana na mkulima wa Tanzania na kumuuliza unafanya kazi badala ya kukuambia yeye ni Mkulima, anakuambia hana kazi.Je hii ni sahihi kweli?.Au unakuta katika zoezi la usajili, mfano mpiga kura, mtu akiulizwa unafanya kazi gani, akisema hana kazi basi anajaziwa kuwa ni Mkulima.Hii ni hatari sana.Je kilimo si kazi?Tafakari.

Nyenzo za kilimo bado nazo ni changamoto kwa mkulima. Pengine hii inaweza kuwa sababu inayomfanya Mkulima anazidi kuwa katika utegemezi licha ya kuelezwa kwamba Kilimo ndiyo sekta ambayo inaweza kuleta mapinduzi ya maendeleo katika jamii.

Pamoja na hayo yote, bado zipo juhudi za kuhakikisha Mkulima wa Tanzania anakombolewa hususani Wakulima wadogo wadogo Wanawake, lengo likiwa ni kuwaondoa wanawake katika umaskini na utegemezi katika jamii.

Miongoni mwa juhudi hizo ni pamoja na uanzishwaji wa Shindano la Mama Shujaa wa Chakula hapa nchini. Shindano hilo huwashirikisha akina mama kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini ambao huonyesha ujuzi wao katika masuala mbalimbali ya kilimo nk.Shindano hilo linadhaminiwa na Shirika la Oxfam.

Mshindi wa Shindano hilo hupatiwa nyenzo mbalimbali za kilimo kwa ajili ya kuzitumia katika kujiletea maendeleo kupitia sekta hiyo ya kilimo. Mwaka 2014 Mshindi wa Shindano la Mama Shujaa wa Chakula alitokea Mkoani Mwanza, katika Wilaya ya Ukerewe na anafahamika kama kwa jina la Bahati Muriga ambae alijinyakulia nyenzo mbalimbali za kilimo zenye thamani ya shilingi Milioni 25.

Washiriki walioshiriki shindano hilo ni Elinuru M. Pallangyo - Arusha, Dorothy D. Pallangyo - Arusha, Leah D. Mnyambugwe - Dodoma, Martina G. Chitete - Iringa, Grace G. Mahumbuka - Kagera, Zinaida J. Kijeri - Kigoma, Upendo M. Msuya - Kilimanjaro, Neema U. Kivugo - Manyara, Elizabeth Simon - Morogoro, Joyce N. Hassan - Mtwara, Bahati Muriga - Mwanza (Mshindi), MS Thereza Kitinga - Mwanza, Santina Mapile - Njombe, Mary A. Ndasi - Rukwa, Fredina M. Said - Shinyanga,  Esther Kulwa - Simiyu, Mary J. Mwanga - Singida, Doricus M. Shumbi - Singida, Kuruthum R. Mwengele - Tanga.
 
Muriga anatarajiwa kukabidhiwa zawadi zake Jumamosi hii ya tarehe 02.08.2014 huko Wilayani kwake Ukerewe. Oxfam inaamini katika kuwekeza kwa wakulima wadogo wanawake kwa kuwa inalipa. Mimi pia naandika Makala hii nikiwa naamini kuwa Kilimo kinalipa. Kinachonisikitisha ni pale ninapoona Mkulima huyu ambae anategewa anazidi kuwa maskini kila kukisha.

Nifikiriavyo mimi Mkulima huyu anazidi kuwa maskini kwa kuwa analima kilimo kisichokuwa na tija kwa kuendelea kuwekeza katika kilimo cha kutumia nguvu badala ya kutumia weledi. Kushiriki katika kilimo cha kisasa.Pili Mkulima huyu wa Tanzania kukosa nyenzo (Pembejeo) bora za kilimo sanjari. Bado naamini katika Kilimo kwanza.Wadau hili mjaribu kulitazama kwa kina ili kilimo cha Mtanzania kiweze kuwa cha maendeleo na sio cha umaskini.Wakulima wawezeshwe pembejeo na elimu pia itolewe kwao na naamini Kilimo Kwanza inawezekana nchini Tanzania.
Na: George Binagi @99.4 Metro FM & Mtanzania Media.

No comments:

Powered by Blogger.