LIVE STREAM ADS

Header Ads

LHRC: TUTAKWENDA MAHAKAMANI KUIPINGA RASIMU YA TATU, KAMA RASIMU YA PILI ITACHAKACHULIWA BUNGENI.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) Jana Kimezindua Kampeni za Kukuza uelewa wa Rasimu ya Pili ya Katiba kwa Wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Uzinduzi huo umefanyika katika Hotel ya JB Belmont Jijini Mwanza.

Ezekiel Massanja (Kushoto) ambae ni Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu akiwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Isaack Ndasa ambaeni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza (Kulia).
Anna Henga (Kushoto) ambae ni Mratibu wa Shughuli za Mabadiliko ya Katiba Mpya kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu akiwa na Ezekiel Massanja (Kulia) ambae ni Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) Kimesema kuwa endapo kama Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba Mpya inayoendelea kujadiliwa Bungeni Mjini Dodoma itachakaguliwa, Kituo hicho kitawahamasisha wananchi kuikataa Rasimu ya Tatu itakayofikishwa kwao kwa ajili ya Kupigiwa Kura.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Mwanza na Anna Henga ambae ni Mratibu wa Shughuli za Mabadiliko ya Katiba Mpya kutoka katika Kituo hicho, wakati akizungumza katika Uzinduzi wa Kampeni za Kukuza Uelewa wa Rasimu ya Pili ya Katiba kwa wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Kama Rasimu ya Pili itachakachuliwa bungeni, tutapiga kampeni ya kuwahamasisha wananchi kuikataa rasimu ya tatu itakayowasilishwa kwao kwa ajili ya kuipigia kura. Na tunaamini watatuelewa maana wakiiona Rasimu ya tatu iliyochakachuliwa wataigundua kwa kuwa tayari tumeanza kuwaelimisha Rasimu ya pili inayojadiliwa bungeni ilivyo” Alisema Henga.

Aidha Henga aliongeza kuwa “Hilo likishindikana na hatimae Rasimu iliyofikishwa kwa wananchi ikapitishwa kuwa Katiba Mpya ili hali tunajua kwamba ilikuwa imechakachuliwa, tutafungua kesi Mahakami kwa ajili ya kuikataa Katiba hiyo”.

Awali akifanya uzinduzi wa Kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza Isaack Ndasa ametoa wito kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa Ujumla kutokuwa tayari kutumika vibaya katika kuuvuruga mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

Katika kuhakikisha tunawafikia wananchi wengi, vyombo vya habari vina wajibu mkubwa mno wa kutumia vyema fursa waliyonayo katika kuwafikishia wananchi ujumbe huu wa Rasimu ya Katiba. Ni vyema wamiliki na wafanyakazi wa vyombo vya habari kuwa na msimamo thabiti juu ya kuwaelimisha na kuwapa wananchi taarifa za ukweli juu ya maendeleo na matokeo ya mchakato mzima kadri unavyoendelea” Alisema Ndasa na kuongeza

“Waandishi wa habari wasikubali kutumiwa kama chombo cha kuchochea na kusambaza chuki na uhasama kwa wananchi. Wajibu wa waandishi wa habari ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu na taarifa sahihi ya Katiba na hatimaye waweze kushiriki vyema katika kupiga Kura ya Maoni”.

Katika hatua nyingine Ndasa pia aliwakumbusha wananchi kwamba mchakato wa Katiba bado unaendelea, na umefikia hatua za mwisho ambazo zinahitaji ushiriki wa kila mmoja hivyo ni vyema wakatambua kwamba mchakato huo wa Katiba ukipita sasa, Katiba itakayopatikana itatumika kwa hivi sasa na baadae kwa vizazi vingi vijavyo, na itachukua muda mrefu sana kabla ya kutungwa Katiba nyingine hivyo akawataka kujitokeza kwa wingi katika kushiriki zoezi la upigaji kura pindi rasimu ya tatu itakapowasilishwa kwao.

Asilimia kubwa ya wadau waliojitekeza katika Uzinduzi wa Kampeni hiyo, walikuwa wakivutana mara kwa mara kuhusiana na mwendendo wa katiba mpya unavyoendelea hivi sasa, ambapo mvutano huo uligawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza likionekana kukubaliana na mchakato unavyoendelea mpaka hivi sasa, huku kundi jingine likionyesha kutoridhishwa kabisa na mchakato huo na kuonyesha wazi wazi kutaka bunge maalumu la katiba linaloendelea mjini Dodoma kuahirishwa badala ya kuendelea kugharibu pesa za watanzania.

Baada ya Uzinduzi wa Kampeni za Kukuza Uelewa wa Rasimu ya Pili ya Katiba kwa Wananchi kufanyika Mkoani Mwanza, Kampeni mbalimbali zitaendelea kutolewa kwa wananchi wa Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Simiyu na Shinyanga. TAIFA NI LETU, KATIBA NI YETU, SOTE TUHUSIKE.
Burudani ya Ngoma mbalimbali zinazohamasisha upatikanaji wa Katiba Mpya nazo pia zilikuwepo katika Uzinduzi huo.
Mkurugenziwa UTPC Abubakar Karsan (Kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye ulemavu wa ngozi Mkoani Mwanza (TAS) Alfredy Kapole (Kulia).
Na: George Binagi @99.4 Metro FM & Mtanzania Media.

No comments:

Powered by Blogger.