Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba toka Kamati namba
Tano, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro akisoma taarifa wakati wa mjadala wa jioni
bungeni hapo jana 15 Septemba, 2014 mjini Dodoma.
|
Hoja ya kusitisha Bunge Maalum la Katiba imehitimishwa rasmi Kisheria kwa
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutamka kwamba bunge hilo
linaweza kuendelea na shughuli zake. Taarifa hiyo imetolewa jana 15
Septemba, 2014 na Mjumbe wa Kamati namba Tano, Mhe. Dkt. Asha-Rose-Migiro
wakati wa mjadala wa jioni bungeni hapo.
Akisoma taarifa hiyo, Dkt. Migiro amesema kuwa
mjadala wa kusitisha bunge
umefungwa rasmi hapo jana licha ya kuwepo kwa madai kuwa bunge hilo halina
uhalali wa kisiasa.
“Kwaajili ya kuondoa shaka yoyote ningependa kuwaambieni takwimu
tulizonazo hivi sasa, bunge hili lina jumla ya Wajumbe 630, kati ya hao
waliotoka ni wajumbe 130 ambao ni sawa na asilimia 21% tu ya wajumbe wote,
wajumbe waliobaki ndani ya bunge ni 500 hii ni sawa na asilimia 79% ya wajumbe
wote na tukizichambua takwimu hizi, ningeomba kutambua wingi wa Kundi la 201”,
alisema Dkt. Migiro.
Akikanusha juu ya kuwepo kwa dhana iliyojitokeza ya kwamba wajumbe
waliobaki ndani ya bunge hilo ni wa aina moja, Dkt. Migiro alisema kuwa taarifa
hizo si za kweli, kwani kati ya wajumbe 500 walioko ndani ya bunge hilo wajumbe
wanaotokana na kundi la 201 ni wajumbe 189 ambapo wajumbe wanaotoka Tanzania
bara jumla yao ni 348 na kati ya hao, 125 ni wajumbe wanaotoka katika kundi
hilo la 201.
“Ukitazama takwimu hizi kwa jicho lolote lile basi wajumbe wa 201 ni
sehemu kubwa na ni sehemu muhimu ya wajumbe hawa waliobaki”, alisema Dkt.
Migiro.
Akizungumzia juu ya wajumbe toka upande wa Zanzibar, Dkt. Migiro alisema
kuwa wajumbe waliobaki ni 152 na kati ya hao wajumbe 64 wanatokana na kundi la
201.
“Tunasisitiza takwimu hizi kwa wajumbe wa 201 kwasababu wajumbe hawa
ndiyo wajumbe ambao kwa wingi wao kitakwimu lakini pia kwa wingi wao kimakundi
wanawakilisha sura zote Kitaifa, hivyo ni dhairi kwamba kwa namna yoyote ile
waliobaki ndani ni wengi, ni idadi kubwa, ni idadi wakilishi na tukiangalia kwa
takwimu hizi, wajumbe walioamua kususia bunge kwa pande zote mbili hizi
hawafikii hata theluthi moja ya wajumbe waliobaki”, alisisitiza Dkt.
Migiro.
Kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, Dkt. Migiro alieleza kwamba uamuzi
upatikane kwa maridhiano, kwa majadiliano na kwa kushawishiana kwa hoja wajumbe
waliobaki na walio wengi wanaweza wakatumia wingi wao na wana uhalali wa
kisiasa na wa kisheria.
Dkt. Migiro aliendelea kusema kuwa, wajumbe waliotoka hawakuona kuwa
utaratibu huo ungekuwa na manufaa kwao licha ya kuwepo na maridhiano katika
bunge hilo, pia kupitia wadau mbalimbali Vyama vya siasa vyote vimekuwa
vinazungumza nje ya bunge kupitia Msajili wa Vyama vya siasa, kupitia Kituo cha
Demokrasia (TCD) na kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete.
|
No comments: