JAMII IVUNJE UKIMYA ILI KUFICHUA UKATILI DHIDI YA WATOTO.
Juhudi mbalimbali za kuhakikisha
kwamba Ukatili dhidi ya Watoto katika jamii unatokomezwa bado zinahitajika
miongoni mwa wanajamii, baada ya kubainika kwamba Watoto walio wengi wanapitia
Vitendo mbalimbali vya Ukatili.
Mkoani
Mwanza Ukatili dhidi ya Watoto unaelezwa kuibuka kila Kukicha huku jambo la
Kushangaza likiwa ni kwamba, Watoto walio wengi wamekuwa wakitendewa Ukatili wa
aina mbalimbali na wanafamilia wenyewe wakiwemo wazazi wao.
Katika Tukio
la hivi karibuni ambalo lilitokea katika Kata ya Buhongwa, Msichana Naomi
Wilson Mwenye Umri wa Miaka 14 ambae ni Mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika
Shule ya Sekondari Twihurumie iliyoko Kata ya Buhongwa Jijini Mwanza, ameelezea
namna alivyonusurika kifo baada ya Mama yake Mzazi kummwagia mafuta ya taa na kisha
kumchoma moto hali ambayo imemuachia majeraha katika maeneo mbalimbali ya mwili
wake hususani Mikononi, Usoni na Shingoni.
Naomi anasema "nakumbuka siku ya tukio ilikuwa usiku majira ya saa mbili
ambapo mama alianza kuniadhibu na hatimae kumwagiza mafuta ya taa na kiberiti kijana wetu wa kazi na kisha kunichoma moto kwa kosa la kunikuta nje usiku huo nikiwa na kijana mmoja ambae ni rafiki yake na kaka".
Naomi
anasema baada ya Mama yake kumtendea ukatili huo, alitorokea kusikojulikana na
hadi sasa inaelezwa kuwa Mama Naomi hajulikani alipo ambapo baada ya tukio hilo
Naomi alifikishwa katika Hospital ya Mkoa wa Mwanza Sekour Toure kwa ajili ya
Matibabu zaidi.
Kwa sasa
Naomi anauguza Majeraha yake katika Kituo cha Kuzuia na Kutokomeza Ukatili dhidi
ya Watoto Majumbani lililopo Kiloleli Mkoani Mwanza la Foundation Karibu
Tanzania, ambapo kiu kubwa ya Naomi anasema kuwa anatamani sana kuonana na mama
yake kwa kuwa amekwisha msamehe na amemkumbuka sana Mama yake pamoja na mdogo
wake.
Hatimae Radio Metro Fm na Binagi Media Group ilifika katika Ofisi za Shirika hilo la Kuzuia na Kutokomeza
Ukatili la Foundation Karibu Tanzania ambapo mtoto Naomi anaishi kwa sasa huku
akiendelea kuuguza majeraha ya moto aliyoyapa baada ya kuchomwa moto na mama
yake mzazi na kuzungumza na Mariagoreth Itovelo ambae ni Afisa Ustawi wa
Shirika hilo ambae alibainisha kwamba hali ya Naomi inaendelea vyema tofauti na
ilivyokuwa hapo awali.
Itovelo
akaeleza kwamba Walifika katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekour Toure Agost
13 mwaka huu ambapo Naomi alikuwa amelazwa kwa ajili ya Matibabu, ambapo
alitibiwa na kuruhusiwa kutoka Hospitalini Agost 24 mwaka huu na kuelekea
nyumbani kwao Buhongwa kabla ya kuchukuliwa na Shirika hilo Agost 28 mwaka huu baada
ya Naomi kuwa na wasiwasi wa kuishi nyumbani kwao akihofia huenda mama yake
angerudi na kumtendea ukatili zaidi.
Katika hatua
nyingine Itovelo anatoa ushauri kwa wanajamii kujenga dhana ya mtoto wa mwenzio
ni wako pia na hatimae kuvunja Ukimya na kufichua matendo ya Ukatili kwa watoto
ambapo anawaasa wanajamii kufikiria mara mbili kabla ya kutenda ukatili wa aina
yoyote dhidi ya watoto.
Nae Abimelick
Richard ambae ni Mwanasheria na Mwezeshaji wa Shirika la Foundation Karibu
Tanzania anasema kuwa bado kuna kasi kubwa ya matukio ya Ukatili dhini ya
Watoto katika jamii, hivyo Shirika hilo linajitahidi kutoa elimu kwa wanajamii
ili kuweza kufichua na hatimae kutokomea Ukatili dhini ya watoto huku
akibainisha kuwa kadri Shirika hilo linavyozidi kutoa elimu katika jamii ndivyo
matukio mengi ya ukatili yanavyoripotiwa kwa kuwa hapo awali matukio mengi ya
Ukatili katika jamii yalikuwa hayaripotiwi.
Katika hatua
nyingine Richard anasema kuwa Shirika hilo linafanya kazi chini ya Kaulimbiu ya
Vunja Ukimya, Fichua Ukatili hivyo wanajamii wanapaswa kuwa tayari kuchukia
vitendo vya Ukatili dhini ya Watoto ambavyo anasema kuwa kwa asilimia kubwa
vimewasababishia watoto walio wengi kupoteza viuongo vya miili yao, huku
akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Shirika hilo
limepokea taarifa za zaidi ya 250 za ukatili mkubwa dhidi ya watoto huku watoto
zaidi ya 2,000 wakiwa wameokolewa baada ya shirika hilo kuingilia kati matukio
ya ukatili waliyokuwa wakitendewa katika jamii.
Hakika ni jukumu
langu, wewe pamoja na yule katika kuhakikisha kwamba vitendo vya Kikatili vya
aina yoyote ile havikubaliki katika jamii, ambapo kubwa zaidi wanajamii wanaasa
kuvunja ukimya na Kufichua Vitendo vya kikatili dhidi ya watoto na hatimae
jamii nzima kwa lengo la kuwa na Familia Salama na Jamii Salama pia.
No comments: