LIVE STREAM ADS

Header Ads

SHIRIKA LA STARKEY HEARING LATOA AHUENI KWA WATU WENYE MATATIZO YA KUSIKIA JIJINI MWANZA.

Wananchi wa maeneo mbalimbali Mkoani Mwanza, wamejitokeza kwa wingi  kufanyiwa uchunguzi wa Masikio, baada ya  Shirika la Starkey Hearing Foundation kutoka nchini Marekani  kutoa huduma hiyo Jijini Mkoani Mwanza bila malipo.

Akizungumza juzi, Mratibu wa huduma hiyo Kanda ya Ziwa Wilfred Serikali alisema  kuwa
idadi kubwa ya wakazi wa Mkoa wa Mwanza wameitikia wito  wa kufanyiwa uchunguzi  kutokana na wengi wao kuathiriwa na matatizo mbalimbali ya Masikio.


 Serikali alieleza  kuwa lengo la kutoa huduma hiyo katika Mkoa wa Mwanza ni kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye matatizo ya masikio hususani viziwi, sanjari na wale ambao masikio yao yanakuwa na  uchafu wa muda mrefu unao wasababishia kutosikia kama vile usahaa na kuziba kwa ngoma ya sikio.



Alisema watu wanaokutwa na matatizo kama hayao, husafishwa na kupatiwa dawa maalumu  zitakazo wasaidia  kusikia vizuri kama kawaida .



“Watu  wanaogundulika kuwa na tatizo la kutosikia, hasa kwa viziwi, tuna kifaa maalumu (Hearing Aids) ambacho hutumia betre kwa muda wa miaka 5, tunawapatia kifaa hicho kila mmoja cha kwake ili kuweza kuwasaidia kusikia”.Alisema Serikali.



Alifafanua kwamba, kifaa hicho  kitawafanya waweze kusikia kama awali, ikiwa ni pamoja na  kuongea na simu, kusikiliza muziki na mada zinazo tolewa darasani na hata katika shughuli mbalimbali za kijamii wanazo zifanya. Huduma hiyo ilianza kutolewa Jijini Mwanza tangu juzi Ijumaa Septemba 19 katika Shule ya Msingi Nyanza na inatarajiwa kufikia tamati leo Septemba 21.


Kwa upande wake Mwalimu wa shule ya viziwi na mvalishaji wa vifaa vya usikivu kutoka Arusha Raphaeli Lukumai, alisema kuwa huduma hiyo inatolewa katika Mikoa mbalimbali  ambapo kwa sasa wapo  Kanda ya Ziwa ambapo tayari wananchi wanaosumbuliwa na matatizo ya kusikia katika Wilaya za Musoma na Bunda Mkoani Mara, wamekwisha nufaika na huduma hiyo



Raphaeli alisema kuwa pamoja na kutoa huduma hiyo maeneo mbalimbali, bado  wanakumbana na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu  kuwa waoga pindi wanapochukuliwa vipimo, baadhi kutokuwa na ngoma ya sikio kutokana  kuchokonolewa mara kwa mara kipindi wanapokua wanatoa uchafu sikioni.

Rachel Daniel ambaye ni  mmoja wa wagonjwa wa kutosikia jijini Mwanza, alieleza kuwa amefurahi kupata huduma hiyo, kutokana na kuwa  awali  alishindwa kupata huduma hiyo muhimu kutokana na kutokuwa na fedha kwa ajili ya kulipia gharama kwa ajili ya matibabu ama kununua kifaa hicho kinachompa mtu asie sikia uwezo wa kusikia.
Katika kuhitimisha ufafanuzi wake, Wilfred Serikali ambae ni Mratibu wa Chama cha Kuhudumia Viziwi Tanzania ( Starkey Hearing Foundation) alieleza kwamba chama hicho kinafanya kazi kwa  kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia wizara ya Afya na Ustawi wa jamii na wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi, ambapo  kambi hiyo ya kutoa huduma kwa watu wenye matatizo ilianzishwaa tangu mwaka 2008 hapa nchini.
Na Prisca Japhes.

No comments:

Powered by Blogger.